Rais MAGUFULI Jipu Lingine Hili Hapa Limeiva!

Magufuli amalizia Baraza la Mawaziri-001Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
NIWAPONGEZE wote waliovuka salama katika kipindi cha Sikukuu ya Pasaka, maana baadhi yetu walikutana na majanga, yawe ya kujitakia au yasiyotarajiwa. Waliokutana na majanga ya kujitakia, ni kama wale walioamini kuwa ili Pasaka ionekane imefika, basi lazima wanywe sana pombe, matokeo yake wakajikuta kwenye aibu, hasara au kashfa.

Baada ya hapo, nieleze masikitiko yangu kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) juu ya kinachoendelea hivi sasa huku mitaani. Wote tunajua kuwa tokea mwaka jana, bei ya mafuta ya petroli na dizeli imekuwa ikishuka baada ya mafuta ghafi pia kushuka katika soko la dunia.

Ingawa mafuta hayo yanashuka bei katika soko la ndani kwa mbinde, maana ushahidi wa mazingira unaonyesha wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) hawapendi bidhaa hiyo ishuke, lakini bado Sumatra inaonekana kama chombo cha serikali chenye kazi ya kuwakandamiza wananchi badala ya kuwa kinyume chake.

Ewura imeshusha bei ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa zaidi ya mara mbili katika kipindi cha miezi sita iliyopita, lakini Sumatra imeendelea kubaki kimya pasipo kutoa tamko la kupunguza nauli kwa mabasi ya mikoani au daladala za mijini. Katika jiji la Dar es Salaam kwa mfano, baadhi ya njia nauli zimeongezwa.

Kadiri muda unavyokwenda, hakuna dalili kama bei hizo zitapunguzwa. Hili ni jambo linalosikitisha na ambalo halikubaliki. Zipo tetesi mitaani zinazowataja baadhi ya wakubwa wa taasisi hizi (Ewura, Sumatra) kuwa na uhusiano unaotia shaka na wafanyabiashara wa mafuta na vyombo vya usafiri, ndiyo maana siku zote wanasimamia zaidi masilahi yao kuliko wananchi.

Tunakumbuka jinsi watu walivyowapigia kelele Ewura kwa kutoshusha bei ya mafuta licha ya bidhaa hiyo kushuka katika soko la dunia. Walitoa visingizio vingi vilivyowafanya wasishushe, hadi wakidai kuwa eti kulikuwa bado na mafuta yaliyonunuliwa kabla bei hiyo haijashuka katika soko la dunia.

Basi angalau hao Ewura wamepunguza, vipi Sumatra hadi leo haijashusha nauli? Uzoefu wetu unatuonyesha kuwa bei za mafuta zinapopanda katika soko la dunia, mamlaka hizi mbili za serikali hupandisha bei za mafuta na nauli haraka, bila kujali kama yapo mafuta yaliyonunuliwa kabla bei haijapanda!


Tunamuomba Rais Dk. John Magufuli kuliangalia suala hili kwa jicho la tatu, maana lengo la serikali yake ni kuwapa unafuu wananchi kwa kadiri inavyowezekana. Haiwezekani bei ya mafuta ishuke halafu nauli iendelee kuwa ileile.

Kutoshusha nauli ni sawa na kuwaibia wananchi maana wenye vyombo vya usafiri wanapata faida kubwa sana. Mafuta yanaposhuka ni lazima watu wa kada zote wafaidi unafuu wake, lakini kuwanufaisha wenye magari peke yao ni kutowatendea haki wadau wengine wa nishati hiyo.

Kama Sumatra hawawezi kushusha nauli za daladala na mabasi ya mikoani, tunaomba mamlaka iliyo juu yao kuwalazimisha kufanya hivyo ili kutimiza ahadi ya rais wakati akiomba kura ya kuondoa kero za wananchi. Haya ni majipu yanayohitaji tiba!
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment