Aliyekuwa Mhasibu Mkuu Wizara Ya Mambo Ya Ndani Katika Jeshi La Kuzima Moto Na Uokozi Na Wenzake Wahukumiwa Kwa Kesi Ya Uhuhujumu Uchumi

Aliyekuwa Mhasibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani katika jeshi la kuzima moto na uokozi na Bw. Naamini Hendry Sangiwa pamoja na Mkandarasi na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiareni Investment Ltd Bw. Webu Manoth Masawe wamehukumiwa leo tarehe 24/3/2016 kwa kesi ya kuhujumu uchumi katika Mahakama ya wilaya ya Ilala. Hukumu hiyo ilisomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mhe. Hassan.
 
Washtakiwa tajwa hapo juu walishtakiwa kwa makosa 7 yakiwemo Matumizi Mabaya ya Madaraka, Kutumia Nyaraka Kumdanganya Mwajiri kinyume na kifungu cha 22 na 31 mtawalia vya Sheria ya kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11/2007, Kughushi Nyaraka kinyume na Kifungu cha 333, 335 (d) (1) na 337 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, na kuisababishia Serikali hasara kinyume na Aya ya 10(1) ya Jedwali la Kwanza, Kifungu cha 57(1) na 60(1) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200.
 
Mnamo mwaka 2009 Serikali ilitoa zabuni ya Ujenzi wa uzio wa Chuo cha Zimamoto na Uokozi kilichopo Mbopo Bunju katika Manispaa  ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam. 
Kampuni ya Kiareni Investment Ltd (Mzabuni), ilipatiwa zabuni hiyo na kulipwa Kiasi cha Shilingi 81, 963, 360/=. 

Hata hivyo taratibu za utoaji zabuni hazikufuatwa, na Mzabuni ambaye ni Kampuni ya Kiareni Investment Ltd, alifanya kazi yenye thamani ya kiasi cha Shilingi 13, 784, 652/= tu kati ya fedha yote aliyolipwa. 
Ili kuwezesha malipo ya Shilingi 81, 963, 360/= kulipwa pasipo kazi kukamilika, Washtakiwa walitoa zabuni kwa Mkandarasi pasipo Mkataba (LPO), na Kughushi Hati ya kuonesha kazi imekamilika (Certificate of Works Completion).
 
Washitakiwa wote watatu walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala mwanzoni mwa mwaka 2014 na kusomewa mashtaka yao Mbele ya Hakimu Mkazi Hassan, ambapo washitakiwa walifunguliwa kesi ya Uhujumu Uchumi No. 06/2014. 
Upande wa Jamhuri katika Kesi hii uliwakilishwa na Wakili STANLEY HILMAR LUOGA akisaidiana na Wakili EMMANUEL JACOB, wote waendesha Mashitaka wa TAKUKURU Makao Makuu.
 Upande wa washtakiwa wote waliwakilishwa na Wakili wa Kujitegemea MDUMA. 

Upande wa Jamhuri uliita Mashahidi 7 na kupeleka vielelezo 21 ili kuthibitisha kesi dhidi ya washtakiwa. Upande wa washtakiwa hawakuita shahidi hata mmoja walijitetea wenyewe.
 
Mshitakiwa wa kwanza Dotto Salehe Mgogo, ambaye alikuwa Kaimu Mkuu wa Mafunzo wa Wizara ya Mambo ya Ndani katika idara ya Jeshi la Zimamoto na Uokozi alifariki dunia mwaka 2014 baada ya kusomewa mashitaka na hivyo Mashitaka dhidi yake yalifutwa kwa mujibu wa sheria. 
Kufuatia kifo cha Mshitakiwa wa kwanza, Mshitakiwa wa Pili Bw. Naamini Hendry Sangiwa ambaye alikuwa Mhasibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani Katika Jeshi la Zimamoto na Uokozi alikuwa anakabiliwa na makosa manne (4) ambapo makosa mawili ni ya Matumizi Mabaya ya Madaraka, Kughushi na Kuisababishia Serikali Hasara, ametiwa hatiani katika makosa yote mawili ya Matumizi ya Madaraka na kupewa adhabu ya kulipa faini ya Tshs.300, 000 kwa kila kosa la Matumizi Mabaya ya Madaraka kama atashindwa kulipa faini, kwenda jela miezi 6 kwa kila kosa.
Katika Kosa la Kughushi Nyaraka, Mshtakiwa ametiwa Hatiani na Kuamriwa kutotenda kosa lolote la jinai kwa muda wa miezi 12.
 
Mshitakiwa wa tatu ambaye ni Bw. Webu Manoth Masawe, ambaye ni Mkandarasi na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiareni Investment Ltd, anakabiliwa na Kosa moja la Kuisababishia Serikali Hasara. 
Mahakama imemtia hatiani na kumpa adhabu ya kwenda Jela miaka mitatu (3) pamoja na Kuirudishia Serikali kiasi cha Shilingi 67, 913, 748/= ikiwa ni hasara aliyoisababishia Serikali.

IMETOLEWA NA OFISI YA AFISA UHUSIANO
TAASISI YA KUZUIA NA KUPAMBANA NA RUSHWA
24 MACHI, 2016
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment