Watu
wawili wameuawa mkoani Shinyanga katika matukio mawili tofauti,
likiwamo la kijana kuchomwa kisu akigombea mwanamke katika baa ya Matunu
mjini Shinyanga.
Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Dismas Kisusi alisema tukio la
kwanza ni la juzi saa 6:00 usiku katika eneo la baa hiyo iliyopo mtaa wa
Kaunda, kata ya Shinyanga Mjini, ambapo mwendesha bodaboda aliuawa kwa
kuchomwa kisu akigombea mwanamke.
Kisusi
alimtaja aliyeuawa kuwa ni Jumanne Ramadhani (22) mkazi wa Ndala katika
Manispaa ya Shinyanga, ambaye alichomwa kisu kifuani upande wa kushoto
na Emmanuel Shombe (20) mkazi wa Majengo na mfanyakazi wa kampuni ya
Mobisolar inayojihusisha na uuzaji wa umeme wa jua.
Akielezea
zaidi kuhusu tukio hilo, Kaimu Kamanda Kisusi alisema chanzo cha tukio
hilo ni Ramadhani kutaka kumchukua kwa nguvu dada wa Shombe, Ester
Shombe (18) mkazi wa Majengo mjini hapa.
“Ramadhani
alikuwa analazimisha kumchukua kwa nguvu Ester ndipo kaka yake aitwaye
Emmanuel akachukua kisu na kumchoma nacho kifuani upande wa kushoto
kulikomsababishia kuvuja damu nyingi, alifariki akiwa njiani kupelekwa
hospitali”, alieleza Kisusi.
Alisema
Polisi inawashikilia watu wanne kwa ajili ya mahojiano zaidi kuhusu
tukio. Wanaoshikiliwa ni Shombe, Ester, Joseph Amos na Tausi Mathias.
Katika
tukio la pili, mlinzi na mkazi wa kijiji cha Isaka Station, wilayani
Kahama, Moshi Saliboko (36) ameuawa kwa kunyongwa huku miguu yake ikiwa
imefungwa kamba umbali wa mita 15 kutoka lindoni kwake katika ofisi za
kampuni ya simu ya Zantel. Kisusi alisema Saliboko aligundulika kuuawa
juzi saa 1:00 asubuhi katika kitongoji cha Majengo, kijijini humo.
Alisema
Saliboko aliuawa kwa kunyongwa huku miguu yake ikiwa imefungwa kamba
kisha wauaji kupora vipande vinne vya betri, rada aina ya 165AH, betri
1PG na transfoma (3CUWENT). Alisema baada ya tukio wauaji walitokomea
kusikojulikana.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment