KAMATI
ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, imemwomba Rais John
Magufuli kuangalia tatizo la uhaba wa sukari nchini na kuona jinsi ya
kufanya kuruhusu kutoa vibali kwa wafanyabiashara kuagiza sukari nje ya
nchi.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo,
Dk Mary Nagu alisema uhaba wa sukari nchini kwa sasa ni kati ya tani
80,000 hadi 100,000 na kwamba kama hatua za haraka hazitachukuliwa,
bidhaa hiyo itahadimika na wananchi watalanguliwa.
“Tumekutana
na Bodi ya Sukari, na tumezungumza nao, wametuambia kuna upungufu wa
sukari ya matumizi ya nyumbani kati ya tani 80,000 hadi 100,000,
tunamuomba Rais na serikali yake kuangalia jambo hili na kuona umuhimu
ya kuruhusu kiasi hicho cha sukari kiingizwe,” alisema Dk Nagu.
Alisema
kabla ya nchi kubinafsisha viwanda vya sukari ilikuwa inazalishwa kwa
mwaka tani 100,000 na baada ya kubinafsishwa viwanda vya ndani
vinazalisha tani 320,000 ilhali mahitaji ni tani 420,000.
Hivi
karibuni, Rais Magufuli alitangaza kupiga marufuku uingizaji wa sukari
kutoka mataifa ya kigeni ili kuvilinda viwanda vya sukari nchini humo
ambavyo vimeathiriwa na uingizaji wa sukari ya bei rahisi kutoka nje.
‘’Tuna
viwanda nchini ambavyo hununua miwa kutoka kwa wakulima wadogo wadogo.
Viwanda hivi huzalisha sukari, ajira na ni chanzo cha mapato ya
serikali. Ijapokuwa tuna hifadhi ya kutosha ya sukari kuna watu
serikalini wanaotoa vibali vya kuingiza sukari kutoka nje,” alisema Dk Magufuli.
Aidha,
Bodi ya Sukari Tanzania ilitangaza kushusha bei ya sukari kwa kutangaza
bei elekezi inayoonesha bidhaa hiyo kuanzia sasa inauzwa Sh 1,800 kwa
kilo nchini kote, huku ikisema haitasita kuchukua hatua stahiki za
kisheria kwa wale watakaobainika kupandisha bei au kuhodhi bidhaa hiyo.
Naye
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwezekezaji, Charles Mwijage alisisitiza
kuwa hakuna uhaba wa sukari nchini na kuwataka wafanyabiashara walio na
leseni za kuingiza na kuuza bidhaa hiyo, kutoificha.
Hata
hivyo, Dk Nagu jana alidai upungufu wa sukari nchini upo na kwamba wapo
wafanyabiashara wanaotumia mwanya huo vibaya kwa kuagiza sukari nyingi
kuliko ile iliyokubaliwa kwa lengo la wao kunufaika, na kuiomba serikali
kuongeza juhudi za kuziba mianya ya uingizaji wa sukari bila vibali.
Alisema
ni vyema serikali ikaona haja ya kuondoa tatizo la uhaba wa sukari hivi
sasa kwa sababu kama uhaba huo utaendelea, wananchi ndio wataathirika
zaidi huku wafanyabiashara akitumia mwanya huo kuongeza bei ya bidhaa
hiyo ila iwapo itaagizwa kwa wakati, si rahisi kwa wafanyabiashara hao
kupandisha bei.
Mkurugenzi
Mkuu wa Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa cha mkoani Morogoro, Hamad Yahaya
anawasihi wafanyabiashara wasio waaminifu, kuacha kutoa taarifa za
uongo kuhusu kiasi cha sukari waliyonayo ili ionekane kuna upungufu na
wao wapandishe bei.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment