Akitoa uamuzi wa hukumu hiyo iliyosomwa jana na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Mwamkuga Gunta, alisema haoni kama kuna kasoro yoyote katika uchaguzi huo uliompa ushindi Laizer.
Akitoa uamuzi, Gunta alisema licha ya Zelote kudai kudhalilishwa pamoja na kuibiwa kura lakini ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mashahidi mbalimbali hautoshi kudai kuwa alipokwa ushindi wa kuwa diwani wa kata hiyo.
“Natupilia mbali kesi hii sababu ushahidi uliotolewa mahakamani hapa hautoshi kumvua udiwani diwani wa Chadema, pia mashahidi waliotoa ushahidi mahakamani hapa ushahidi wao umejichanganya hivyo natupilia mbali kesi hii,” alisema Gunta.
Awali kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo wiki iliyopita, Hakimu Gunta aliomba radhi kwa kutokamilisha hukumu hiyo kwa sababu alikuwa akiuguliwa hivyo aliahidi kutoa hukumu jana, Machi 29.
Kesi hiyo ambayo awali ilisikilizwa kwa siku mbili mfululizo kwa zaidi ya saa nane kila siku, mashahidi wote walikamilisha ushahidi wao akiwamo Laizer aliyekiri mahakamani hapo kuwa aliongozana na kundi kubwa la wafuasi wa chama chake kwenda katika kituo kikuu cha kujumlishia matokeo ya udiwani katika kata hiyo kilichokuwa katika shule ya sekondari ya Musa.
Hata hivyo, akiongozwa na wakili wake Adiel Charles, diwani huyo alishindwa kukanusha lugha ya matusi iliyotolewa na wafuasi wake aliyokuwa ameongozana nao Oktoba 25 mwaka jana, wakiwa na silaha za jadi ambazo ni sime na fimbo pamoja na kutishia usalama wa maisha ya mgombea wa CCM, Zelote.
Wengine waliotoa ushahidi wa upande wa mlalamikiwa ni pamoja na msimamizi msaidizi wa uchaguzi kata ya Musa, Tuwati Leondoya.
Wengine ni Lomito Robert na Ally Mollel. Kwa upande wa mlalamikaji, mashahidi watano walitoa ushahidi akiwamo Zelote, Meimoite Kivuyo, Lekisongo Singa, Edson Lesikari na Alex Lukumay.
Kesi hiyo ya uchaguzi namba sita ya mwaka 2015 ilifunguliwa mahakamani hapo na Zelote aliyekuwa mgombea wa udiwani katika kata hiyo kwa tiketi ya CCM dhidi ya Laizer wa Chadema.
Zelote alifungua kesi hiyo baada ya kubaini kuwapo kwa ukiukwaji mkubwa wa taratibu za kampeni pamoja na uchaguzi zilizotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Laizer alitangazwa mshindi katika uchaguzi huo.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment