Nianze na nukuu hizi mbili kuntu za Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere- Mwenyezi Mungu amrehemu.
“Democracy is not a bottle of Coca-Cola which you can import. Democracy should develop according to that particular country”. June 1991 in Rio De Janeiro, Brazil
"Demokrasia
sio chupa ya Coca-Cola ambayo unaweza kuagiza. Demokrasia lazima ikue
na kuendelezwa kulingana na nchi husika". Juni 1991 Rio De Janeiro,
Brazil (Tafsiri ni yangu)
“No
nation has the right to make decisions for another nation; no people
for another people”. From ‘A Peaceful New Year’ speech, Tanzania,
January 1968
"Hakuna
Taifa lina haki ya kufanya maamuzi juu ya Taifa lingine; wala watu juu
ya watu wengine ". Hotuba ya Amani ya Mwaka Mpya, Tanzania, Januari 1968
(Tafsiri ni yangu)
Hili
la Marekani na uamuzi wa MCC ni jambo la mpito na haliwezi kuua
mahusiano yetu na Marekani. Tanzania na Marekani zinashirikiana kwa
mambo mengi na MCC ni sehemu tu tena ni eneo jipya la ushirikiano.
Uamuzi
huu ni jaribio kwa uhuru wa Taifa letu. Hakuna namna nyingine ila
kushinda hili kama tulivyoshinda mengine huko nyuma. Kwa wale ambao
wameuona umri watakumbuka namna tulivunja uhusiano na Ujerumani
Magharibi 1964 pale walipotaka kuwa na kauli hasi dhidi ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar.
Tulivunja
uhusiano na Ujerumani Magharibi baada ya kutaka kuingilia Uhuru wa
Mataifa Mawili huru yaliyoamua kuungana na kuunda Nchi Mpya ambayo leo
tunajivunia, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
1965
Tulivunja uhusiano na Uingereza kufuatia na kitendo cha wazungu
wachache kujitangazia Uhuru (Unilateral Declaration of Independence)
kule Rhodesia na uingereza kukaa kimya na kushindwa kuchukua hatua
stahiki.
Tulivunja
Uhusiano na Uingereza kuieleza Dunia kwamba Uhuru wa nchi za Afrika ni
kipaumbele muhimu kwa Tanzania. Jambo tunalopaswa kufahamu ni kuwa MCC 2
toka mwanzo imekuwa ni mtihani dhidi ya uhuru wetu.
Napenda
ieleweke kwamba kipindi hiki kilichotokea sio kuvunjika kwa uhusiano
wetu na Marekani bali taasisi ya MCC ndio imesitisha msaada wao kwetu,
lakini mahusiano yetu na marekani bado yako pale pale, na si Marekani au
Tanzania inayoweza kuugharimu uhusiano wetu.
MCC
1 ilikuwa ni chambo cha kutuvuta na tulipewa bila masharti tena hela
nyingi dola milioni 698 na ni fedha tulizopewa moja kwa moja na kupewa
uhuru wa kuamua tuzitumieje.
Tanzania
ilitakiwa kuainisha maeneo kisha wao wanatoa hela. Ndio maana miradi
kama ile barabara ambazo hazikuwa zikipata ufadhili kwa kuwa
hazikuonekana ni za kiuchumi na miradi ya maji ya Morogoro na kwingineko
iliingizwa humu na kupata ufadhili.
MCC 2 sio hivyo. Kwenye MCC 2 walengwa wakubwa ni sekta binafsi ya Marekani, hapa kuna mtego hapa, hapa ni biashara hapa.
Mchakato
wa MCC 2 ulipoanzishwa, wafanyabiashara kwa kushirikiana na Maseneta
wakaanzisha hoja kuwa kwanini Marekani inatoa fedha kwa ufadhili katika
nchi ambazo China ndio wenye kufaidika na fedha hizo?
Wakaleta
hoja ya kuwa Serikali ya Marekani ifanye jitihada ya kuweka fedha kwa
kusaidia Sekta Binafsi ya Marekani kupenya Afrika.
Ukaitishwa
mkutano wa US-Africa Summit na agenda kubwa ikawa Power Africa. Katika
Power Africa, Marekani ikalichagua eneo la Nishati (si uzalishaji
viwanda) kwa kutambua kuwa ndio eneo pekee wanaloweza kushindana na
wachina.
Wakasema
wataelekeza fedha huko kuisaidia Afrika kutatua tatizo la nishati
ambalo ndio pembejeo ya viwanda. Wakaweka sharti kuwa fedha hizo na
miradi hiyo itatekelezwa na Sekta Binafsi ya Marekani.
Ndio
sababu wengi wenu mtakumbuka hata Rais Obama alitangazia dhamira ile
pale Ubungo kwenye Mitambo ya Symbion Power na sio kwamba alipenda
kwenda kutembea Ubungo.
Kuanzia
hapo kumekuwepo na shinikizo kubwa sana na masharti magumu na yenye
kuhamahama (shifting goal post) kutaka kuibaka sekta ya nishati nchini
ikiwemo mageuzi ya TANESCO.
Zikaainishwa
hatua kadhaa,ambazo utekelezaji wake baadhi ni kisheria na kisera na
hivyo haziwezi kwenda kwa deadline walizotaka.
Kila
bodi ikikutana wanaibua hiki na kile lakini wakisema hela watatoa. Hela
hizi zikawa zimeshikiliwa kama chambo ukisogelea zinasogea, ni sawa na
ule mchoro wa Mpanda Punde aliyeshika fimbo yenye majani na akiielekeza
mbele ya punda, kwamba punda ataendelea kuyafuata majani akidhani
atayafikia kumbe ndio anaupiga mwendo.
Hatimaye
wakasema wanasubiri uchaguzi mkuu jambo ambalo halihusiani na madai ya
mwanzoni. Baada ya uchaguzi wakaibuka na suala la Zanzibar.
Hivyo,
uamuzi wao wa leo ni uamuzi uliotarajiwa. Pia ni uamuzi wenye madhara
kwa sekta binafsi ya Marekani pia ambayo ndio ilikuwa itekeleze miradi
hiyo.
Kama
Taifa ni muhimu kulinda utu na uhuru wetu. Ndio msingi wa sera yetu ya
nje toka mwanzo na hata sasa. Tumetofautiana na Marekani katika hili
tutapatana katika mengine. Ndio uhai wa maisha ya diplomasia.
Wao
nao wanayo hadhira ya wapiga kura wao wanayojaribu kuituliza huko
nchini kwao kwa uamuzi huu. Tunapaswa kuheshimu uamuzi wao kama ambavyo
wanapaswa kuuheshimu wetu.
Hatimaye
baadae tutapatana. Marekani inaihitaji Tanzania zaidi na Tanzania
inaihitaji Marekani. Marekani inahitaji MCC 2 zaidi hali kadhalika
Tanzania inahitaji MCC 2.
Mahusiano ya Tanzania na Marekani hayakuanza na hayataisha na MCC. MCC imeyakuta na itayaacha.
Kama
marudio ya uchaguzi wa Zanzibar ndio kigezo, basi Marekani isingekuwa
inatoa zaidi ya Dola Bilioni 3 kila mwaka kwa Egypt iliyo chini ya
utawala wa kijeshi kwa sababu ya kuununua ugomvi wa Egypt na Israel na
isingetoa kiasi cha dola bilioni 6 kwa Israel kila mwaka kwa yale
wanayoyafanya dhidi ya Wapalestina.
Huu
ni wakati ambao Taifa linawaita Wazalendo wake. Wazalendo wasimame na
kusema 'Nchi yangu KWANZA, iwe Sahihi au Imekosea" na Makuwadi
watashangilia na kusema "si mnaona sasa kiko wapi?".
Huu
ni wakati wa kujifunga mikanda na kulinda heshima yetu kama Taifa letu.
Tuna vyanzo vya mapato vingi sana ambavyo hatujaanza kukusanya mapato,
tuwe wabunifu na tusibweteke na kutegemea mapato yataongezeka maradufu
kwa vyanzo vile vile.
Niseme
kwa uchache, sababu walizotoa MCC, na ieleweke aliyetoa tamko ni MCC,
heri lingetoka tamko hili Wizara ya Mambo ya Nje au Ikulu ya Marekani,
moja ni Zanzibar na pili ni Sheria ya Makosa ya Mitandao (Cyber crimes
Act).
Sasa hebu tujadili kidogo, hivi kule Zanzibar tulitaka kitokee nini pale ambapo wanasiasa walikuwa hawataki kujadiliana?
Tume
ile ile ya Uchaguzi ambayo bado ilikuwa na uhalali wa kikatiba na
kisheria kuuitisha, kuufuta na kuuitisha tena uchaguzi ikachukua nafasi
yake.
Wanasiasa
wasio makini wakaishia kuhamishia malumbano mitandaoni badala ya
kuitafuta suluhu ya kisiasa na pale siasa iliposhindikana basi
wangeitafuta suluhu katika mahakama za Zanzibar.
Mezani
wakashindwa, mahakamani hawakwenda. Tume ikachukua uongozi, uchaguzi
ukaitishwa Wananchi wakapiga kura na sasa huko Zanzibar kuna serikali na
baraza la wawakilishi.
Hata
mimi sifurahii sana njia waliyoichukua Zanzibar lakini ilibidi siasa za
madaraka zisite ili tuanze kufanya siasa za maendeleo. Je wamarekani
walitaka muujiza gani utokee huko.?
Kuhusu
Sheria ya Mitandao, hata mimi siipendi, si twende mahakamani, bunge
litaanza vikao muda si mrefu je wabunge si wapeleke hoja ya kuifanyia
marekebisho sheria hii.
Sasa Marekani (MCC) inapoweka shinikizo kwa suala la Sheria ambayo ni jambo la ndani na linaloweza kujadilika, sijaelewa.
Mbona
sie hatujapiga kelele Yule jamaa yao Trump alipotutusi waafrika na
kusema sisi stahili yetu ni kuwekwa tena chini ya ukoloni (hapa
nimechomekea tu).
INDHARI
Ni
aibu kwa viongozi wa kisiasa kufurahia jambo hili, ni ishara ya ukuwadi
wa kisiasa na ambao uko tayari kukumbatia mahusiano yanayotweza Uhuru
wetu. It is now high time kufanya siasa safi za maendeleo (politics of
development) na sio kujikita katika katika siasa za madaraka (Politics
of Power).
*************
Imeandikwa na: Humphrey Polepole.
Mwandishi,
Ndg. Humphrey Polepole amenufaika na uelewa wa watu wenye uzoefu wa
mahusiano ya Tanzania na nchi za Nje. Aidha, ni mnufaikaji (alumni) wa
programu ya uongozi chini ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment