Wabunge Waiponda Bajeti Ya Viwanda

Wajumbe wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira wamekerwa na kiwango cha bajeti ya Sh95. 6 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, wakisema haionyeshi malengo ya Tanzania kuelekea kuwa nchi ya viwanda.

Wabunge walisema hayo baada ya Waziri Charles Mwijage kuwasilisha taarifa ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa 2016/17 mbele ya kamati.

Waziri Mwijage alisema kati ya fedha hizo, Sh 53.5 bilioni (sawa na asilimia 56), zimetengwa kwa matumizi ya kawaida wakati Sh42.1 bilioni (asilimia 44) ni kwa ajili ya maendeleo.

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Hawa Subira alisema wakati wa kujadili taarifa hiyo kuwa kiwango hicho kinaonyesha wazi jinsi Serikali isivyo na nia ya kufufua viwanda kama alivyoahidi Rais John Magufuli.

“Homa ya Magufuli inawaogopesha. Nakuonea huruma waziri (kwa kuwa) unaonyesha kabisa kuwa una nia njema, lakini kwa mtindo huu lazima uumwe,” alisema Subira.

“Tafuteni panadol tuwasaidieni. Tunataka nchi hii kweli iwe ya viwanda. Hatuwezi kufanya kazi namna hii watu mmejaa uoga hata kupanga bajeti ya kueleweka mnashindwa au mkikaa mnaogopa kurekodiwa,” alisema.

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alisema nchi kuwa ya viwanda na biashara inawezekana, lakini Serikali inapaswa kudhihirisha kwa vitendo badala ya maneno kwa kuwa wizara hiyo ilipaswa kutengewa fedha za kutosha kuonyesha njia ya kuelekea kwenye malengo yaliyokusudiwa, kama kuruhusu safari za nje ya nchi kwa maofisa wa wizara kwa nia njema.

“Lakini kuna mambo yamekuwa yakifanyika ya ajabu. Mimi naweka mambo ya siasa pembeni. Serikali iangalie upya hii bajeti, lakini pia huo mradi wa China Logistics Centre hauna msaada kwa nchi badala yake utaua hata viwanda vidogo vidogo vilivyopaswa kusaidiwa kuinuka. Hatuwezi kuifanya Dar kuwa Dubai wakati viwanda vya ndani havijaimarishwa,” alisema.

Kwa upande wake mbunge wa Nkenge(CCM), Dk Diodorus Kamala alisema wakati mwingine Serikali imekuwa ikiwapa wapinzani kauli kutokana na mambo inayofanya. 

Alisema kiwango hicho cha fedha hakiendani hata na taarifa aliyoiyoa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango hivi karibuni alipowasilisha mapendekezo ya mpango wa bajeti.

“Fedha ni ndogo wakati tunatakiwa tujikomboe kwa kupiga hatua za kimaendeleo kutoka hapo tulipo. Mfano naona wizara imeridhika kuwa pale kwenye jengo la Water Front, badala ya bajeti hii kueleza mpango wake wa kujenga ofisi ya kujitegemea ili kusaidia hata kupunguza matumizi,” alisema.

Akijibu hoja hizo, Mwijage alisema haoni tatizo kwa kiwango cha bajeti alichotengewa kwa kuwa malengo ya wizara yake kwa mwaka huu wa fedha pamoja na mambo mengine ni kuboresha mazingira ya viwanda vilivyopo kisha mwaka ujao ndipo watajikita kujenga vipya.

“Ninachokiona hapa ni kwamba wengi wanataka kuona nchi inakuwa hivyo leo, kumbe tunatakiwa kuanzia kwa kuboresha mazingira ya hivi vilivyopo kwani vingi vinazalisha chini ya asilimia 50 kutokana na vikwazo mbalimbali ikiwamo miundombinu duni,” alisema.

Katika mapendekezo ya mpango wa bajeti ya 2016/17, Serikali imeweka fedha nyingi katika kuboresha miundombinu ya usafiri kama reli, barabara na viwanja vya ndege, uzalishaji wa nishati ya uhakika, hasa umeme unaotokana na gesi na makaa ya mawe na kuboresha rasilimali watu kwa ajili ya kuweka mazingira wezeshi ya kukua kwa viwanda.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment