Waziri Sospeter MUHONGO Asisitiza Mapinduzi ya Kiuchumi katika Sekta ya Nishati na Madini

Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Sospeter Muhongo amelishauri Baraza la Wafanyakazi wa Nishati na Madini kujikita katika kujadili mwelekeo wa mapinduzi ya kiuchumi kwa kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye viwanda.
 
Mhe. Muhongo aliyasema hayo jana Jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo, ambapo baadhi ya mambo yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni masuala ya usafiri kwa wafanyakazi wa wizara hiyo, upandishwaji vyeo kwa wafanyakazi, mafunzo pamoja na uhaba wa nafasi wa ofisi kwa wafanyakazi.
 
Kuhusu suala la upandishwaji vyeo, Mhe. Muhongo alisema kuwa tayari yeye kama Waziri alishafanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ili kuona namna gani wafanyakazi wanapandishwa vyeo kulingana na elimu pamoja uwezo wao kikazi ambapo alipendekeza kubadili mtindo wa upandishwaji vyeo uliopo sasa kwani ni wa zamani.
 
‘’Sifa za upandishaji vyeo kwa wafanyakzi ni vema ukabadilika pamoja na muda wa utoaji vyeo, hivyo napenda kuwasisitiza kuwaangalia vijana tulio nao kwani pale Wizarani tuna vijana wengi wazuri wenye uwezo mkubwa katika kufanya kazi. Katika kikao hiki ni vema mkajadili namna gani mnawapa kipaumbele vijana katika kuwapandisha vyeo vijana hawa,’’ alisema Muhongo.
 
Kuhusiana na uhaba wa nafasi za ofisi, Mhe. Muhongo alifafanua kuwa, ofisi nyingi za Serikali ziko katika mfumo wa zamani, hivyo amelishauri Baraza hilo kuona namna gani watabadilisha muundo wa ofisi ili watu wakae pamoja katika eneo moja lililo wazi na kufanya kazi kuliko kila mtu kuwa na sehemu yake ya kufanyia kazi hali inayosababisha ufinyu wa eneo na uvivu.
 
Aidha, Amewataka wajumbe wa Baraza hilo kujadili ni namna gani wanaweza kubadilisha hali ya kiuchumi toka asilimia 7% hadi kufikia asilimia 8% mpaka 10% ili kukuza uchumi wa nchi na kutokomeza umasikini.
 
‘’Jukumu kubwa la Wizara ya Nishati na Madini ni kuhakikisha kuwa tunakuza uchumi wa nchi kwa kuhakikisha kuwa kunakuwa na umeme mwingi wa bei nafuu na wa uhakika, na kazi tuliyonayo hapa ni kuongeza uzalishaji wa umeme toka Megawati 1400 hadi kufikia Megawati 5,000 mpaka 10,000 na ikiwezekana hadi 15,000 baada ya miaka 10 ijayo’’, aliongeza Mhe. Mhongo.
 
Kuhusu suala la Mafunzo kwa wafanyakazi hao, Mhe. Muhongo alisisitiza kuwa hakuna mtu anayekatazwa kupatiwa mafunzo kwa maana ya kuongeza elimu juu ya jambo fulani, isipokuwa kuna utaratibu wa kwenda kusoma, ambapo panapotokea umuhimu wa wafanyakazi kwenda kusomea mambo muhimu yenye manufaa kwa umma nafasi hizo ni vema zikatolewa ili nchi iwe na wataalam mbalimbali katika nyanja mbalimbali.
 
‘’Hii Wizara inahitaji watu wasome na waelimike, hivyo tunahitaji watu wasome na wawe wataalam katika maeneo mbalimbali ya kazi lengo likiwa ni kuleta maendeleo ya nchi’’, Alisema Mhe. Muhongo.
Aligusia masuala ya Bajeti katika Wizara yake ambapo alifafanua kuwa zaidi ya asilimia 89.5/% ya bajeti itatumika katika kufanya shughuli za maendeleo ya nchi.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment