SALMA
Kikwete, Mke wa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete ameonesha kukerwa na wale
wanaoshambulia utawala wa mumewe (Rais Kikwete) na kwamba, hakuna sababu
ya kufanya hivyo.
Mama Salma alisema hayo jana kwenye mkutano wa Umoja wa Wanawake (UWT) unaofanyika mjini Dodoma katika ukumbi wa mikutano wa CCM Makao Makuu.
Alitoa
kauli hiyo ikiwa ni siku moja baada ya kujitokeza hadharani kumkingia
kifua mtoto wake Ridhiwani Kikwete kuhusu kuhusika kwake na mkataba
wenye utata wa Kampuni ya Lugumi.
“Kila
mwaka naendelea kuisemea serikali iliyopo madarakani mambo mazuri,
acheni hali ya kukaa na kuanza kusema kwamba serikali ile ilikuwa vile
na serikali hii iko hivi.
“Wala
msisema yule alikuwa vile na huyu yuko hivi, kwa kumalizia hayo napenda
kusema mume wangu ambaye ni mwenyekiti wa CCM Taifa anawasalimia sana,” alisema Mama Salma.
Akizungumzia utumbuaji wa majipu alisema,
serikali kwa sasa imeanza kutumbua majipu makubwa kuanzia juu lakini
zipo taarifa kuwa, yapo majipu mengine ngazi za chini pia ndani ya CCM.
Alisema, “kila
anayejitambua kuwa ni jipu kabla hajafikiwa ni bora akajitumbua
mwenyewe au ajipake spriti ili jipu hilo lipoke mapema kabla
halijatumbuliwa.”
Hata hivyo alionesha
wasiwasi kuwa, kuna uwezekano miradi mingi ya UWT ikachukuliwa kutokana
na umoja huo kuwa na mali ambazo zinaonekana kumilikiwa bila kufuata
taratibu.
Alisema,
kwa upande wa ardhi kuna viwanja vingi ambavyo havina hati na vimekaa
muda mrefu bila kuendelezwa jambo ambalo kwa sasa mameya wanaweza
kuvibadilishia matumizi.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment