WAZIRI
Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, maarufu kama Mtoto wa Mkulima, ameamua
kuishi maisha tofauti kabisa na watangulizi wake kwa kukwepa kukaa
jijini Dar es Salaam na kwenda kijijini kwake baada ya kustaafu.
Pinda
aliwahi kukiri kwamba hana nyumba jijini Dar es Salaam zaidi ya kibanda
kidogo kilichoko Pugu, ambacho hakina hadhi ya kuishi mtu.
Mtoto
huyo wa mkulima amejichimbia katika kijiji cha Makanyagio, Mpanda
mkoani Katavi, akiendesha shughuli za kilimo na ufugaji, tofauti kabisa
na watangulizi wake ambao baada ya kustaafu waliendelea kuishi jijini
Dar es Salaam.
Tangu
awamu ya nne ilipoondoka Ikulu Novemba 5, mwaka jana, Pinda hajawahi
kufanya safari yoyote nje ya nchi na wala kujihusisha na shughuli za
kitaifa na kijamii kama walivyokuwa watangulizi wake.
Aidha, Mizengo Pinda amepotea kwenye vyombo vya habari kama watangulizi wake.
Mtoto
wa Mkulima ni jina ambalo alijipachika mwenyewe baada ya kuteuliwa na
Rais Mstaafu Jakaya Kikwete mwaka 2008 kuwa Waziri Mkuu.
Pinda
alikuwa Waziri Mkuu kati ya mwaka 2008-2015 akichukua nafasi iliyoachwa
wazi na Edward Lowassa (2006-2008), aliyejiuzulu kwa kashfa ya kampuni
ya kufua umeme ya Richmond.
Wakati
Salim Ahmed Salim, baada ya kustaafu, aliendelea kuishi kwenye makazi
yake Masaki na Unguja, John Malecela naye aliendelea kuishi Sea View,
Upanga.
Fredrick
Sumaye baada ya kustaafu nafasi hiyo mwaka 2005 aliendelea kuishi
jijini Dar es Salaam maeneo ya Kiluvya, wakati Lowassa bado ana makazi
Masaki.
Jaji
Joseph Warioba, ambaye naye aliwahi kuwa Waziri Mkuu, aliendelea kuishi
nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam baada ya kuondolewa
kwenye nafasi hiyo mwaka 1990.
Hata
Waziri Mkuu mstaafu, hayati Rashid Kawawa aliweka makazi yake ya kudumu
eneo la Madale jijini Dar es Salaam na ndiko alikozikwa alipofariki
Desemba 2009.
Cleopa Msuya anaendelea kuishi kwenye makazi yake yaliyoko Upanga, jirani na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Pinda
alikuwa miongoni mwa wanachama 42 wa CCM waliochukua fomu za kuwania
kuteuliwa na chama chao kusimamishwa kuwania urais kwenye Uchaguzi Mkuu
wa mwaka jana.
Lakini
bahati haikuwa kwake kwani ni miongoni mwa makada ambao majina yao
yalikatwa mapema na Kamati Kuu ya chama hicho, hivyo kutofanikiwa hata
kuingia kwenye tano bora.
Wanachama
wa chama hicho walioingia kwenye tano bora walikuwa Rais John Magufuli,
January Makamba, Benard Membe, Dk. AshaRose Migiro na Amina Salum Ali.
Tangu
kukatwa jina lake kwenye hatua za awali, Pinda alionekana kujitenga
kabisa na masuala ya siasa na kuamua kuishi maisha tofauti na wenzake
baada ya kustaafu.
Januari
14, 2010 Pinda alitangaza mali anazomiliki kuwa ni Sh. milioni 25
kwenye akaunti yake, nyumba tatu za kawaida moja ikiwa jijini Dar es
Salaam, Mpanda na Dodoma na gari moja alilolinunua kwa mkopo wa Ubunge.
Waziri
Pinda aliamua kufanya hivyo ili kuweka bayana mali zake na kuonyesha
mfano kwa viongozi wote nchini kufata nyayo kwa kuwa viongozi walitakiwa
kuweka bayana mali zao ili kutekeleza sheria ya maadili ya uongozi.
Pinda alisema haelewi maana ya utajiri na kwamba mali alizotaja zimeshamtosheleza.
"Nina nyumba Dodoma ninayojenga kwa mikopo ya nyumba za serikali," alisema Pinda mwaka huo na kueleza zaidi:
"Nina
nyumba Mpanda ambayo imepatikana kwa mpango wa kawaida tu, imetokana na
visenti kidogo nikanunua pale ambapo bahati nzuri gharama za ujenzi
hazikuwa kubwa sana, nikakikarabati kipo pale kipo Makanyagio pale.
"Haya!
Ukitoka pale unataka niseme nini tena. Dar es Salaam sina nyumba ya
kusema ya maana sana ukienda shambani Pugu kule kipo kinyumba kidogo
hivyo inahitajika kazi ya ziada kuweza kufanya paonekane pa maana.
"Kijijini
kwa baba yangu pale Kibaoni sina nyumba; pale mlipoona nimekaa na bibi
tunapiga porojo, kile kijumba mimi na wadogo zangu tulimsaidia babu kwa
ajili ya kumjengea babu yetu na pale ndipo nilipokuwa nafikia siku zote
wakati wa likizo."
Pinda,
ambaye alikuwa Mbunge tangu mwaka 2000 mpaka 2015, alisema miaka yote
alikuwa akifikia kwenye nyumba hiyo ambayo yeye ana chumba chake kimoja
hali kadhalika babu yake.
Alisema
baada ya kuwa Waziri Mkuu, alijikuta kwenye wakati mgumu sana kwa kuwa
alitaka kuendelea kufikia kwenye nyumba hiyo, lakini watu wa usalama
walimkataza.
"Nilipoteuliwa
kuwa Waziri Mkuu nikataka nifikie katika ile nyumba, lakini nikaambiwa
hapana, haiwezekani; hapafai; huwezi kufikia pale," alisema.
Alisema
hilo ndilo lilikuwa tatizo lake la kwanza kwa hiyo atajaribu kujenga
tena kitu ambacho na yeye atapata mahala pa kufikia pamoja na wasaidizi
wake kwenye eneo hilo wakati huo.
"Nimegundua
tatizo ni hawa wakubwa. Pale kijijini kwetu hakuna nyumba za wageni
hatuna chochote mi nilidhani nikienda kule nikiachwa kwa babu na bibi,
wao wataenda huko umbali wa kilomita wakatafute pa kupumzika, lakini
wakasema no! no! no! haiwezekani, nikawaelewa."
Alisema ukiondoa nyumba hiyo, vitu vya maana zaidi hana labda gari la mkopo akiwa Mbunge.
"Hivi ukiwa na hivi nilivyo navyo unahitaji nini cha zaidi tena?
"Kwa
hiyo kipato kidogo unachokipata unaweza kukitumia kwa ajili ya huduma
za watoto wako kusoma na kadhalika kwa sababu ni vitu viko nje ya
taratibu za serikali.”
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment