Wakati Rais John Magufuli akitarajia kuwasili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) leo, wanafunzi walioandamana wakishinikiza malipo yao ya fedha za kujikimu juzi, huenda wakakumbwa na hatua za kinidhamu.
Wanafunzi hao huenda wakaadhibiwa kwa kosa la kukikuka sheria ndogo ya chuo kwa kuandaa mkusanyiko pasipo kibali cha menejimenti.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma), Florens Luoga alisema jana kuwa, mamlaka za nidhamu chuoni hapo zinaendelea na uchunguzi kubaini nani aliyehusika katika tukio hilo.
“Taratibu na sheria ndogo za chuo haziruhusu mtu kuandaa mkusanyiko ambao haujaidhinishwa na menejimenti. Taratibu hizo lazima ziheshimiwe ili ziendelee kuwa imara. Hivyo tunasubiri ripoti ya waliohusika,” alisema Luoga.
Juzi, wakati wa maandamano ya wanafunzi hao walikuwa wakipaza sauti iliyotolewa na Rais Magufuli wakati wa kampeni za kuwania wadhifa huo akisema:
“Serikali yangu haitarajii kuona mwanafunzi akifukuzwa chuo kwa kosa la kugoma kisa mkopo, bali ikitokea mgomo, watawajibisha maofisa wa Bodi ya Mikopo kwa kuchelewesha fedha.”
Taarifa zilizopatikana jana zilieleza kuwa fedha za wanafunzi hao zimeshawekwa kwenye akaunti zao, juzi jioni.
Rais wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo, Erasmi Leon alisema licha ya wanafunzi hao kukiuka utaratibu, haoni sababu za kuwachukulia hatua kwani hawakusababisha madhara wala uharibifu wowote.
“Endapo kamati ya nidhamu itaamua kufanya hivyo ni vyema wakafanya suala hilo kimantiki na kibinadamu na endapo usimamizi wa sheria ukifuata zaidi unaweza ukasababisha kuibuka kwa mambo mengine tofauti,” alisema Leon.
Alisema wanaendelea kuwasihi wanafunzi kuhakikisha suala hilo halijitokezi tena kwani linaitia doa Serikali yake, uongozi wa chuo na Taifa kwa jumla.
Wanafunzi hao waligoma kuanzia Jumatatu usiku na mgomo wao kuisha juzi, baada ya kupewa fedha zao ambazo zilichelewa kwa madai ya uhakiki wanafunzi hewa unaondelea.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment