Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma Matatani.. Waziri Mkuu Majaliwa Aagiza Achunguzwe

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bw. Jordan Rugimbana kuchunguza ni kwa nini Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma Bw Antonino Kilumbi amekwenda kutengeneza madawati kwa watu binafsi badala ya karakana ya Magereza kama ilivyokusudiwa na Serikali.
Magereza mkoa wa Dodoma ilipewa sh. milioni 24 na Serikali ili kutengeneza madawati 480 na kila moja lilitakiwa kugharimu sh. 50,000. Uongozi wa gereza hilo ulitengeneza madawati hayo kwa watu binafsi ambapo dawa moja limegharimu sh. 70,000.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Jumatano, Oktoba 5, 2016 wakati alipotembelea Gereza la Isanga mkoani Dodoma akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo yanayotoa huduma za jamii mjini hapa.

Alisema kama gereza hilo halikuwa na uwezo wa kutengeneza madawati hayo kwa nini kazi hiyo wasingeipeleka kwenye taasisi nyingine ya umma, hivyo amemtaka Mkuu wa Mkoa Bw. Rugimbana kufuatilia ziada ya sh. 20,000 kwenye utengenezaji wa kila dawati inatoka wapi na inakwenda kwa nani.

“Nimesikia kwamba mnawachangisha askari kiasi kilichoongezeka kwenye utengenezaji wa madawati hayo. Ni marufuku askari kutoa fedha mifukoni mwao kulipia shughuli za Serikali,” alisisitiza.

Serikali imeandaa utaratibu wa kuwezesha taasisi zake zikiwemo za kijeshi kwa kuzipa kazi ya kutengeneza bidhaa na miundombinu mbalimbali ikiwemo madawati ili kuyaongezea tija aliongeza

Kwa upande wake Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma Bw. Kilumbi alisema waliamua kupeleka kazi hiyo kwa watu binafsi kwa sababu hawana vifaa.

Aidha, Waziri Mkuu alimtaka mkuu huyo wa magereza mkoa kuimarisha kitengo cha ufundi seremala na kuhakikisha anatumia vizuri nguvu kazi aliyonayo katika kuzalisha bidhaa mbalimbali.

Kuhusu changamoto ya makazi kwa askari Waziri Mkuu alisema Serikali inatambua na imeweka mkakati wa wa ujenzi na kwa upande wa askari Magereza wataanzia kwa mkoa wa Dodoma.

Wakati huo huo Waziri Mkuu alitembelea maduka ya kuuzia bidhaa mbalimbali zikiwemo nguo katika maeneo ya soko la Sabasaba na Majengo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment