Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Kigoma, inawahoji
viongozi wa vyama vitatu vya ushirika vya msingi vya mazao na masoko
(Amcos) mkoani humu kuhusu tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.
Viongozi
hao wanadaiwa kujikopesha Sh mil 500 kinyume na makusudio ya vyama
hivyo. Hata hivyo, inaelezwa kuwa, uchunguzi utaendelea kwa vyama
vingine 17 vya akiba na mikopo, ambapo viongozi wake tayari
wamekwishaanza kufuatiliwa na taasisi hiyo kuhusu tuhuma mbalimbali
zinazowakabili.
Mkuu
wa Takukuru mkoani hapa, Mussa Misalaba, akizungumza na waandishi wa
habari jana alisema, vyama hivyo vinavyotokana na wakulima wa tumbaku
katika tarafa ya Nguruka wilayani Uvinza ni miongoni mwa vyama
vilivyopata mkopo kutoka Benki ya CRDB, kwa ajili ya wanachama wake.
Mkopo
huo kwa mujibu wa Misalaba, ulilenga kusaidia ununuzi wa pembejeo za
kilimo, ujenzi wa mabani ya kukaushia tumbaku na gharama za upangaji
madaraja na ununuzi wa kuni katika msimu wa kilimo wa 2015/2016.
Vyama
ambavyo viongozi wake wanatuhumiwa na kuhojiwa ni pamoja na Matendo
AMCOS, Sagara na Nyangabo, vyote kutoka tarafa ya Nguruka wilayani
Uvinza.
Hata
hivyo, Misalaba alisema baada ya kila mwanachama kuainisha kiasi
alichokuwa anataka na kupatiwa mkopo huo na benki, baadhi ya viongozi na
wajumbe wa bodi wa vyama hivyo, walikiuka taratibu za uendeshaji na
utoaji wa mikopo hiyo, ambapo watu wachache walijikopesha fedha hizo
huku idadi kubwa ya wakulima ikikosa .Inaelezwa kuwa, jambo hilo lilizua
malalamiko miongo ni mwa wanachama.
Akizungumzia
hali hiyo, Ofisa Tarafa ya Nguruka,Thomas Sangai alisema, kitendo cha
viongozi hao kujikopesha fedha hizo, kinaathari kwa wakulima kwani
wakati wa marejesho fedha hizo zitalazimika kukatwa katika mauzo ya
wakulima hao.
Sambamba
na hilo, imeelezwa kuwa vitendo vilivyofanywa na viongozi hao
kujikopesha fedha hizo na kushindwa kuwafikia wakulima huenda
vikasababisha wakulima kutorosha tumbaku na kuuza katika masoko yasiyo
rasmi.
Hatua hiyo inahofiwa kuwa huenda ikachangia kupungua kwa mapato ya halmashauri, yanayotokana na ushuru wa tumbaku.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment