Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa ametishia kufuta halmashauri zitakazoshindwa
kukusanya mapato kufikia asilimia 80 ya lengo na kuwaonya watumishi wa
halmashauri hizo wenye kampuni za uwakala wa kukusanya kodi na tozo
mbalimbali, kutozipa kampuni zao kazi hiyo kuepuka mgongano wa
kimaslahi.
Majaliwa alisema endapo mtumishi wa halmashauri atabainika kutumia kampuni yake kukusanya kodi atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Alisema
hayo jana mjini Dodoma, wakati akifungua mkutano mkuu wa Jumuiya ya
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT).
Kwa
mujibu wa Waziri Mkuu, Serikali ya Awamu ya Tano imejikita katika
uboreshaji wa huduma za wananchi na ukusanyaji mapato, hivyo halmashauri
itakayoshindwa kukusanya mapato kwa asilimia 80 itafutwa.
Alisema
kumekuwa na ufujaji mkubwa wa mapato kupitia mawakala na watumishi
wachache wasio waaminifu. Alitaka mapato yote ya halmashauri yakusanywe
na kusimamiwa vizuri kwa njia za kielektroniki kwa kuwa ndio njia
salama.
“Njia za kielektroniki ni salama na itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza upotevu wa mapato,” alisema.
Alisema,
mkakati wa kuwezesha halmashauri kuwa na miradi na uboreshaji wa
ukusanyaji wa mapato lazima uheshimiwe hasa wakati huu ambao Serikali
inasisitiza umuhimu wa kujitegemea yenyewe.
“Niwakumbushe
watendaji wote, tukibaini taarifa za watumishi wa halmashauri kumiliki
kampuni za kukusanya ushuru na tozo mbalimbali, hatua za kinidhamu
zitachukuliwa. Ni dhahiri kuwa huko ni kuleta mgongano wa kimaslahi,” alisema.
Aliongeza
kuwa, rushwa imekuwa ikilalamikiwa na wananchi katika maeneo yote
hususan kwenye huduma za afya, elimu, ardhi na utoaji leseni mbalimbali
katika Serikali za Mitaa.
“Wananchi
wanakosa haki zao na maisha yao yanaendelea kuwa duni kutokana na hali
iliyojitokeza ya dhuluma, ufisadi na jeuri wanayofanyiwa na watoaji na
wapokeaji wa rushwa. Rushwa ni kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa
majukumu ya maendeleo ya halmashauri, Serikali Kuu na taasisi mbalimbali
za umma,” alisema Majaliwa.
Aliwataka
viongozi wa halmashauri kuikomesha kwa kuwa inalalamikiwa kwenye maeneo
yao na kuondoa ubadhirifu katika ukusanyaji wa mapato, matumizi mabaya
ya madaraka na kukomesha utekelezaji wa miradi chini ya viwango.
Aliwataka
viongozi wakuu kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha hakuna
huduma inayotolewa kwa kutoa rushwa. Pia, alisema Serikali itaendelea
kuimarisha misingi ya kikatiba na namna ya mgawanyo wa madaraka kati ya
Serikali Kuu na za mitaa, lengo likiwa kuhakikisha mipango wanayosimamia
inaleta manufaa kwenye maeneo yao.
“Wakuu
wa mikoa na wilaya wana uwezo wa kuhoji chochote hakuna zuio, lakini
hatujaruhusu Mkuu wa Wilaya kuomba fedha, anatakiwa akague miradi na
ajiridhishe kuwa inatekelezwa ipasanyo kwa thamani ya fedha
inayotengwa,” alisema.
Alisema,
Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya hahitaji posho kwenye vikao vya
halmashauri hivyo wasiogope kuwaalika kwenye vikao vyao. Akizungumzia
migogoro ya ardhi, Majaliwa alisema, imekuwa mingi hali inayotoa somo
kuwa sasa Watanzania wanajua thamani ya ardhi.
Alisema
ili kuondoa migogoro iliyopo, lazima kila halmashauri iwe na mipango ya
matumizi bora ya ardhi kuanzia vitongojini mpaka vijijini. Alitaka
wananchi waitambue mipaka yao kwa sababu hiyo si kazi ya Waziri bali ni
ya halmashauri yenyewe na kila kijiji.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment