WAZIRI
Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa
amesema vitendo vya dhuluma, ufisadi na jeuri vinavyofanywa na watoaji
na wapokeaji rushwa vinasababisha wananchi kukosa haki zao na maisha yao
kuwa duni, hivyo amewataka wajumbe na Viongozi wa Jumuiya ya Tawala za
Mitaa Tanzania (ALAT) kupiga vita rushwa katika ngazi zote za utawala
kwenye mamlaka zao na kwa nchi.
“Sote tunakumbuka msemo wa rushwa ni adui wa haki na kwamba sitapokea wala kutoa rushwa,”
amewasisitiza juu ya umuhimu wa msemo kwa sababu kuna dalili kwamba
rushwa ni kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa majukumu ya maendeleo
katika ngazi mbalimbali zikiwemo za halmashauri, serikali kuu na taasisi
mbalimbali za umma.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo mchana wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa
uchaguzi wa ALAT uliofanyika mjini Dodoma ambapo amesema vitendo vya
rushwa vinalalamikiwa sana na wananchi, katika maeneo yote, hususan
katika huduma za afya, elimu, ardhi na utoaji leseni mbalimbali katika
Serikali za Mitaa.
“Kutokana
na ukweli huo, wapo wananchi ambao wameanza kupoteza imani kwa serikali
yao kutokana na kuendeleza vitendo vya rushwa miongoni mwa jamii.
Natoa wito kwenu mkiwa wajumbe wa chombo hiki muhimu kupiga vita vitendo
vyote vinavyoashiria rushwa katika ngazi zote za utawala kwenye mamlaka
zenu na kwa nchi yetu,” amesema.
Amesema
hata wakati Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.
John Pombe Magufuli anazindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
tarehe 20 Novemba, 2015 alibainisha maeneo mbalimbali ambayo ni kero kwa
Wananchi mojawapo ni tatizo la rushwa miongoni mwa jamii.
Waziri
Mkuu, Majaliwa amesema kuwa wakati wa kampeni za uchaguzi rais alipata
fursa ya kusikiliza malalamiko mengi ya wananchi ikiwa ni pamoja na
kushindwa kwa serikali za mitaa kutekeleza majukumu yake na kuwajibika
kwao kama katiba, sheria na sera zinavyoelekeza.
Amesema
changamoto nyingine aliyoizungumzia Mheshimiwa Rais ni upotevu wa
mapato na kushindwa kukusanya kodi, ubadhirifu, matumizi mabaya ya fedha
na madaraka, ambapo utekelezaji wa baadhi ya miradi upo chini ya
viwango huku kukiwepo na wizi, uzembe katika mamlaka za serikali za
mitaa. hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa fedha.
Waziri
Mkuu, Majaliwa amesema kuna uvujaji mkubwa wa mapato yanayokusanywa na
mamlaka za serikali za mitaa kupitia mawakala au hata baadhi ya
watumishi wachache wasio waaminifu, ambapo alitumia fursa hiyo
kuwasisitiza usimamizi mzuri wa mapato ya halmashauri na kuhakikisha
yanakusanywa kwa njia ya kielektroniki ambapo imebainika kuwa ni salama
na itasaidia kupunguza kupovu huo.
“Ninatambua
kwamba bado zipo changamoto za utaratibu huu wa kukusanya mapato kwa
njia ya elektroniki. Aidha, zipo taarifa kuwa, baadhi ya watumishi wa
halmashauri ndiyo wenye kampuni za uwakala wa kukusanya kodi na tozo
mbalimbali za halmashauri, hivyo nawakumbusha watendaji wote kwamba
taarifa hizi zikibainika ni za kweli, hatua za kinidhamu zitachukuliwa.
Ni vyema wahusika waache tabia hiyo mara moja kwani ni kinyume na
maadili ya utumishi wa umma,” amesema.
Katika
hatua nyingine Waziri Mkuu, Majaliwa ameyataka mabaraza ya Madiwani
yafanye kazi zake kwa mujibu wa sheria, ambapo amekemea tabia ya baadhi
ya watendaji wa halmashauri kutokutaka kuulizwa chochote na mabaraza
hayo kwa kisingizio kwamba wao ni watalaamu.
Amesema
Mabaraza ya Madiwani ndiyo mamlaka ya wananchi katika kusimamia
halmashauri hivyo kuwazuia Madiwani kuhoji chochote hata pale ambapo
wataalam wamekwenda kinyume na maadili ya taaluma na utumishi wa umma
siyo sahihi kiutendaji, hivyo amewataka watendaji hao kuyaachia Mabaraza
hayo yafanye kazi zake na kwa mujibu wa sheria.
Kwa
upande wakea Naibu Waziri wa Nchi, Osisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, Suleiman Jafo amesema watahakikisha wanatoa maelekezo
wanazisimamia vizuri halmashauri katika ukusanyaji wa kodi kwa mfumo wa
kielektroniki.
Pia
Jafo amempongeza Waziri Mkuu Majaliwa kwa utendaji wake na kwamba
amewathibitishia Watanzania kuwa Rais Dk. John Magufuli hakukosea katika
uteuzi huo na kwammba umakini wake katika kuchapakazi umeleta tija
nchini.
Kwa
upande wake Makamu Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Steven Muhapa akitoa
hutuba ya shukurani kwa Waziri Mkuu, amesema maelekezo na maagizo yote
yaliyotolewa na Waziri Mkuu wameyapokea na wataenda kuyafanyia kazi.
Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment