Waziri Mkuu Asema Ahadi zote Zilizotolewa Wakati wa Kampeni Zitatekelezwa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesisitiza kuwa ahadi zote zilizotolewa kipindi cha kampeni mwaka jana pamoja na zilizoko kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zitatekelezwa kama zilivyoahidiwa.

Pia amesisitiza kuwa kupitia ahadi hizo, wamedhamiria kutekeleza kwa vitendo ujenzi wa barabara zote kwa kiwango cha lami na kwa sasa wanatarajia kuanza na barabara zinazounganisha mikoa.

Kauli hiyo ilitolewa na kiongozi huyo bungeni Dodoma jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Nachingwea, Hassan Masala (CCM) aliyebainisha kuwa katika moja ya ahadi zilizopo kwenye ilani ya CCM ni pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami.

Mbunge huyo alihoji, je Serikali ya Awamu ya Tano imejipangaje katika kutekeleza ahadi hiyo? Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema CCM kupitia ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2015, imebainisha ahadi mbalimbali ambazo chama hicho kimeamua zitekelezwe katika kipindi cha miaka mitano.

Alisema pamoja na ahadi ya ujenzi wa barabara katika kiwango cha lami, ahadi zote zilizomo kwenye ilani hiyo zitatekelezwa kama zilivyoahidiwa. 
“Ni kweli kwamba tumedhamiria kujenga barabara zetu kwa kiwango cha lami. Na tumeanza na mkakati wa kuunganisha barabara kwa ngazi ya mikoa, tukishakamilisha tunaingia kwenye barabara zinazounganisha wilaya,” alisema. 

Alisema pia barabara zote zilizoainishwa katika ilani hiyo ya CCM katika awamu hiyo ya tano, zitakamilishwa kupitia bajeti itakayopitishwa na Bunge hilo ya mwaka 2016/17.
“Naomba niwashawishi waheshimiwa wabunge muipitishe bajeti hii ili tuweze kukamilisha barabara ambazo mmezitaja sana humu ndani. Pale ambapo barabara za mikoa hazijakamilika tunataka tuzikamilishe,”alisema.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment