Mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi Enterprises uliosababisha kashfa ya
ufisadi wa mabilioni ya fedha katika Jeshi la Polisi, leo unatarajiwa
kuwasilishwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Mkataba huo huenda ukawasilishwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini
(IGP), Ernest Mangu, ili kutoa fursa kwa wajumbe wa kamati hiyo kuupitia
kipengele kwa kipengele kabla ya viongozi wa jeshi hilo kuanza kuhojiwa
juu ya ufisadi huo.
Kupitia mkataba huo wa 2011, Kampuni ya Lugumi Enterprises ilipewa
tenda ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya
polisi 108 nchini kwa gharama ya Sh bilioni 37.
Tayari kampuni hiyo imekwishalipwa Sh bilioni 34 sawa na asilimia 99
ya fedha zote, huku ikiwa imefunga mashine katika vituo 14 tu katika
jiji la Dar es Salaam ambavyo pia havijulikani vipo maeneo gani.
Uwasilishwaji wa mkataba huo ni utekelezaji wa agizo la PAC, ambapo
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Aeshi Hilaly alitoa siku sita kwa
Jeshi la Polisi kuwasilisha mkataba huo.
Jana Aeshi alisema baada ya kamati yake
kupokea mkataba huo wajumbe wataupitia na kuujadili kwa kina ili kuona
kama kuna upungufu.
“Kesho (leo) ndiyo tarehe 11, tutapokea mkataba kama tulivyowaomba
watuletee, wakituletea tutausoma na kuujadili kwa kina kisha tutawaapa
maelekezo,” alisema Aeshi.
Alisema iwapo kamati yake haitaridhishwa na maelezo ya viongozi wa
Jeshi la Polisi kuhusu mkataba na fedha zilizotumika, upo uwezekano
mkubwa wa kuundwa kwa kamati maalumu.
“Kama vifaa vimefungwa katika vituo vyote, ni matumaini yetu vitakuwa
vinafanya kazi, huwezi kufunga vifaa ambavyo ni vibovu…kama maelezo
tutakayoyapokea hayataridhisha kuna uwezekano wa kuundwa kwa kamati ya
uchunguzi,” alisema Aeshi.
Hivi karibuni Kamati ya PAC ilibaini kuwapo kwa viashiria vya ufisadi
katika Jeshi la Polisi kwa kuwaeleza waandishi wa habari kuwa Kampuni
ya Lugumi ililipwa Sh bilioni 34 kati ya Sh bilioni 37 za mkataba wote.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment