Hali
si shwari ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutokana na mchakato
unaoendelea wa kumkabidhi Rais Dk. John Magufuli uenyekiti wa chama
hicho, kukumbwa na sintofahamu.
Taarifa
kutoka ndani kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC),
kilichofanyika juzi Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma, zimethibitisha
kutokea mgawanyiko wa vigogo ndani ya chama hicho.
Hali
hiyo imekuja baada ya kutokea kwa mvutano juu ya tarehe rasmi ya
kufanyika kwa mkutano mkuu maalumu uliopangwa Juni mwaka huu, ambao
pamoja na mambo mengine Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais mstaafu
Jakaya Kikwete atakabidhi kijiti kwa Rais Magufuli.
Chanzo
cha kuaminika ndani ya kikao hicho kilidokeza kuwa, kabla kilifanyika
kikao kidogo kilichokuwa na wajumbe wanne ambao pamoja na mambo mengine
walijadili ajenda muhimu ikiwamo ya kupanga tarehe kwa ajili ya mkutano
huo.
Kwa
mujibu wa chanzo hicho, kikao hicho kidogo kilishirikisha viongozi
wanne akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho Jakaya Kikwete, Rais Dk. John
Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana.
Habari hizo zinaeleza kuwa, katika kikao hicho kidogo viongozi hao walikubaliana wakatangaze tarehe rasmi, na Rais Magufuli alikubali kukabidhiwa uenyekiti wa chama kama ulivyo utaratibu wa CCM lakini baada ya kikao cha Kamati Kuu kuanza, Kikwete alikataa kuruhusu hoja hiyo ijadiliwe, hatua iliyozua mfarakano.
“Baada
ya kumalizika kwa kikao kile viongozi hao wanne waliingia ndani ya
kikao cha CC ambacho kilikuwa na ajenda kadhaa ikiwemo ya mkutano mkuu
maalumu ambapo mwenyekiti alirusha na kutaka hoja ya tarehe isijadiliwe,” kilisema chanzo hicho.
Kwa
mujibu wa chanzo hicho, ilipofika ajenda ya tatu ambayo iliwasilishwa
na Katibu Mkuu, Kinana kuhusu kutangazwa kwa tarehe ya mkutano mkuu
maalumu, Kikwete aligoma isijadiliwe na badala yake aliahirisha kikao na kutoka nje.
Chanzo
hicho kilisema, uamuzi wa Mwenyekiti Kikwete wa kuahirisha kikao
ulijikita katika suala la gharama za mkutano ambazo zinakadiriwa kuwa ni
zaidi ya Sh bilioni mbili, hivyo aliwataka wajumbe waahirishe kikao ili
kutoa fursa ya kutafuta fedha.
Taarifa
hizo zilieleza kuwa, kutokana na hali hiyo yaliibuka makundi mawili,
moja linalomuunga mkono Kikwete na jingine linalopingana na hoja hiyo,
likidai kuwa fedha si tatizo kwa chama hicho kwa kwani kina miradi,
ruzuku na marafiki wengi.
“Wanaompinga
mwenyekiti walishangazwa na hoja hiyo wakisema kuwa, suala la fedha ni
la watendaji wa chama na si la mwenyekiti, kitendo ambacho wamekitafsiri
kwamba mwenyekiti hana dhamira ya dhati ya kukabidhi chama kwa sasa,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo
hicho kiliendelea kutoa taarifa kuwa, baada ya Kikwete kugoma kujadili
tarehe alisimama mjumbe Jenista Mhagama, ambaye alipinga uamuzi huo,
huku akisema suala hilo ni lazima lijadiliwe kwa kina na tarehe ya
mkutano mkuu itangazwe.
“Kauli
ya mwenyekiti inaonekana iliwaudhi baadhi ya wajumbe, lakini Jenista
alizungumza vizuri sana na kumhoji mwenyekiti inakuaje hataki kusema
lini utafanyika mkutano mkuu maalumu ili akabidhi chama.
“Maana
suala la makabidhiano ni la utamaduni wa ndani ya CCM, Jenista alisema
aliyekaa muda mrefu alikuwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere pekee
lakini na yeye alikabidhi kwa mzee Mwinyi (Ali Hassan) na pia ilipofika
wakati kama huu mzee Mwinyi naye alikabidhi kwa mzee Mkapa.
“Si
hilo tu hata mzee Mkapa naye alikabidhi chama kwake (Jakaya Kikwete),
sasa inakuwaje yeye leo hataki kufuata utaratibu huo ambao ni wa kawaida
ndani ya chama?,” kilihoji chanzo hicho.
Chanzo kingine cha habari kilisema kuwa
baada ya mwenyekiti huyo wa CCM taifa kuahirisha kikao hicho juzi,
aliondoka na kurejea jijini Dar es Salaam kwa gari tofauti na ratiba
iliyokuwa imepangwa.
“Ratiba
ya chama ilikuwa baada ya kikao cha jana (juzi) mwenyekiti angelala
Dodoma na badala yake alipoahirisha kikao kwa utata alipanda kwenye gari
na kuondoa hali ya kuwa alitakiwa kurejea Dar leo (jana).
“Baada
ya kikao hicho alitoka mzee Kinana akiwa amekasirika sana, tena huku
akiwa amekunja sura, unajua siku zote mzee Kinana anaamini kwamba kile
kilichokuwa kinapiganiwa na chama hivi sasa ndicho kinachotekelezwa na
Rais Magufuli tena kwa vitendo tofauti na huko nyuma,” kilisema chanzo chetu.
Baraza la Wazee kukutana
Taarifa
nyingine zinaarifu kwamba, kutokana na hali hiyo Baraza la Wazee la
CCM linaloundwa na viongozi wastaafu, linatarajiwa kukutana kati ya leo
na kesho kwa lengo la kujadili hali hiyo ili kuondoa mtanziko huo
uliojitokeza.
“Ninachotaka
kukuambia katika kipindi cha siku mbili baraza la ushauri la wazee
litakutana na kujadili hali hii na baada ya hapo watakwenda kwa
mwenyekiti kumshauri juu ya uamuzi wake na autafakari kwa kina.
“Tunajua
tunakwenda vizuri katika hili na hakuna kitakachoharibika na wazee wetu
watamshauri vema mwenyekiti ili kupata mwafaka wa kudumu na mkutano
mkuu utafanyika mwezi uliopangwa,” chanzo hicho kilisema.
Baraza
la Ushauri la Wazee wa CCM, linaongozwa na Rais mstaafu wa awamu ya
pili, Ali Hassan Mwinyi (Mwenyekiti), Pius Msekwa (Katibu) na wajumbe ni
Rais mstaafu Benjamin Mkapa pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM mstaafu
(Bara), John Malecela.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment