Madaktari Wawili na Muuguzi Wasimamishwa Kazi Kwa Kumtolea Lugha Chafu Mjamzito Aliyejifungulia Chooni

Hospitali ya Rufaa ya Amana, Ilala imewasimamisha kazi madaktari wawili na muuguzi mmoja, kwa madai ya kumtolea lugha isiyostahili mjamzito Asha Said (17), aliyejifungulia chooni.

Tukio hilo lilitokea mwezi uliopita katika hospitali hiyo, baada ya Asha kujifungulia chooni na madaktari na wauguzi hao kumtolea lugha chafu, bila kuelezwa sababu za kufanya hivyo.

Mganga Mkuu wa Amana, Dk Meshack Shimwela alisema jana kwamba watumishi hao ambao hakuwataja wamepelekwa katika Baraza la Watumishi na Madaktari la hospitali hiyo kwa uchunguzi zaidi.
“Kilichotokea siku ile ni kauli zilizotoka kwa watumishi hao kwenda kwa mama aliyejifungua, ambaye pia alikuwa mdogo kiumri.

“Sisi madaktari na waaguzi tuna taratibu za kinidhamu, huwa tunazifuata baada ya watumishi kubainika kufanya makosa, hatua ya kwanza ndiyo hiyo tusubiri nyingine wakati uchunguzi ukiendelea dhidi yao,” alisema Dk Shimwela.

Dk Shimwela ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), alisema kilichohitajika ni lugha nzuri kwa sababu kisheria ni lazima kwa mgonjwa yeyote kuoga akifika hospitali, ili kumkinga na maradhi mbalimbali.

Wakati hayo yakitokea Amana, Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) kimeitaka jamii kuendelea kuibua matukio ya unyanyasaji na huduma mbaya wanazofanyiwa na wakunga wakati wa kujifungua, ili vyombo vinavyohusika viweze kuliona tatizo kwa ukubwa wake na kulifanyia kazi.

Akizungumza katika kongamano la siku mbili la kujadili maendeleo ya wakunga nchini, rais wa chama hicho, Feddy Mwanga alisema kila wanaposikia malalamiko kuhusiana na unyanyasaji na huduma mbaya kwa wajawazito, chama hicho hufanya utafiti na kuchukua hatua stahiki kwa wahusika.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment