Rais wa Simba, Evans Aveva.
Khadija Mngwai Dar es Salaam
RAIS wa Simba, Evans Aveva, amesema wanasubiria ripoti ya kocha Mganda, Jackson Mayanja ili kujua iwapo watamuongeza mkataba au la. Mayanja alipewa mkataba wa muda mfupi wa kuinoa Simba ambao unatarajiwa kufikia tamati mwishoni mwa msimu huu, baada ya kuondoka kwa Muingereza Dylan Kerr.
Hata hivyo, Mayanja alieleza kuwa, kuna timu kadhaa zinamfuatilia za hapa Tanzania na nje ya Tanzania na kudai kuwa yupo kikazi na anakaribisha mazungumzo na timu yoyote, japokuwa anaipa nafasi ya kwanza Simba.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Aveva alisema wanasubiri ligi ifikie tamati ili waweze kukaa chini na Mayanja kuzungumza ili kujua iwapo watamuongeza mkataba mwingine au la.
“Tunasubiri ligi itakapofikia tamati ndiyo tukae naye chini kwa kuangalia ripoti yake inasemaje ndipo tuamue la kufanya. Tunajua kocha anaweza kuwa na mipango yake, hivyo kila kitu kitajulikana huko mbele baada ya ligi kuisha.
“Kuhusu kuwa na mipango ya kuwa na kocha mwingine, bado haijajulikana na siwezi kusema chochote, kwa sasa tunaelekeza nguvu zetu kwenye ligi,” alisema Aveva.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment