Nchemba ameyasema hayo jana mchana, baada ya kuwasili nyumbani kwa marehemu, Mbezi Beach, barabara ya Bagamoyo mtaa wa Makonde alipofika kusalimia ndugu pamoja na waombolezaji.
Alitumia fursa hiyo kukaa na wanafamilia na ndugu waliohudhuria hapo kabla ya kutoa maneno machache kwa jinsi anavyomfahamu marehemu Christina.
“Msiba hauna itikadi za vyama, msiba unatuhusu wote, na hawa ni ndugu zangu toka Singida, na huyu marehemu ni mtu wangu wa karibu nimefanya naye kazi kwenye kamati ya bajeti, yeye akiwa naibu msemaji wa Wizara ya eEdha, kweli ni mtu makini aliyetanguliza maslahi ya taifa badala ya maslahi binafsi.” Alisema Mwigulu
Aliongeza kwamba, marehemu alikuwa ni mtu anayeweza kushauri ukweli na ushauri mzuri hivyo kifo chake ni pengo kwa taifa, kwa chama chake na watu wa Singida ambao amewatumikia kwa miaka mitano kwa nafasi yake ya Ubunge wa viti maalumu.
Tofauti na ilivyotarajiwa kwa sababu za utani wa Wanyiramba (kabila la Mwigulu) na Wanyaturu (Kabila la Lissu), Mwigulu alikuwa mstaarabu hakuingiza utani kwenye msiba kama ilivyozoeleka kwa makabila yanayotaniana humu nchini.
Alitumia muda mrefu kuongea na dada mkubwa wa Lissu ( Mama Kabula) kabla ya kukaa na wazee, kuwapa pole, kutoa rambirambi na kuwaaga.
Wakizungumza baada ya kuondoka kwa Waziri huyo, baadhi ya Wazee kutoka Singida walimsifu kwani wamekuwa wakihasimiana bungeni lakini kwenye suala la msiba, ameonyesha hakuna itikadi za vyama na ameshirikiana na ndugu zake toka Singida, jambo waliloita ni ukomavu wa siasa.
Christina, amefariki dunia Aprili 8 mwaka huu, anatarajiwa kuagwa katika viwanja vya Karemjee, Jumanne, Aprili 12 na kuzikwa nyumbani kwao wilaya ya Ikungi Aprili 13, siku ya Jumatano.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment