Serikali
imeeleza kusikitishwa na uamuzi wa Marekani kusitisha uhusiano katika
Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), bila kuishirikisha wala
kuisikiliza.
Kadhalika,
imesema hakuna umuhimu wa misaada ya afya na elimu inayofadhiliwa na
Marekani kwa dola za Marekani milioni 700 (Sh. trilioni 1.5), kama
imejitoa katika kusaidia miradi ya umeme ambayo ni muhimu katika
utekelezaji wa miradi inayofadhili, kwa kuwa ni sawa na kutoa kwa mkono
wa kulia na kupora kwa mkono wa kushoto.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, baada ya kupokea
taarifa ya uamuzi wa MCC, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga, alisema
uhusiano na Marekani utaendelea katika maeneo mengine, lakini kwa fedha
hizo hakuna la kufanya ingawa milango iko wazi iwapo watafikiria upya.
“Fedha
ni zao, uamuzi ni wao wameutoa Washington. Hatuwezi kulia kwa ajili ya
hili, tutaendeleza ushirikiano katika maeneo mengine, lakini tunawaomba
wafanye uchambuzi wa kigezo cha demokrasia kwa asilimia 100
kinachotumika katika misaada hiyo,” alibainisha na kuongeza:
“Wametusaidia
kwa miaka mitano kwa vile tulikidhi vigezo, ila sasa tumeshindwa kimoja
inafuta imani na uelewano ambao ulikuwapo kati yetu. Nishati ndiyo
nyenzo ya maendeleo kwa Tanzania. Kwa sasa tunaelekeza umeme vijijini
ili vijana wanaosoma bure wajisomee na hospitali zitoe huduma muda
wote.”
Waziri
Mahiga alisema Tanzania imetia saini mkataba wa malengo ya milenia
ambayo yanakwenda sambamba na MCC, hivyo kufuta fedha hizo kwa sasa ni
sawa na kuumiza mahali panapouma zaidi huku ikiwa (Marekani) kiongozi wa
utawala bora, demokrasia na soko huria duniani.
Alifananisha
kunyimwa fedha hizo sawa na kutoa adhabu kwa mkosaji bila kujali kuwa
alipaswa kumwelimisha na kumwonya kabla ya adhabu kubwa.
“Ukichukua
mizani na kuweka nyama upande huu na jiwe upande mwingine, ukapima
mazuri ambayo Tanzania imekuwa ikifanya na kuonekana mtoto mzuri machoni
mwa dunia, lakini upungufu wa sasa waliouona, utaona tuna mazuri mengi,
hivyo hatukustahili adhabu hii,” alisisitiza.
“Uamuzi
wao hatuwezi kuwaingilia, nasi tukiamua yetu wasituingilie.
Tumejitahidi tuwezavyo kulinda demokrasia na hatutarudi nyuma kwani
katika uchaguzi wa Zanzibar vyama vilishirikishwa. Waelewe na kutambua
mazuri yetu tunayofanya na tutaendelea kufanya,” afafanua.
Aidha,
alisema suala la Zanzibar liliendeshwa vizuri kwa kuwa lilitoa nafasi
ya mazunguzo kwa pande zote na kwamba hakuna mwenye uwezo wa kuingilia
masuala ya uchaguzi, serikali na mambo ya ndani ya visiwa hivyo kwa kuwa
wana katiba na sheria zao bali mambo machache tunashirikiana na hata
Rais Dk. John Magufuli, alikuwa mwangalizi tu.
Balozi
Mahiga aliishangaa Marekani kwa kueleza kuwa uamuzi wa sasa unapingana
na tamko la hivi karibuni lililosisitiza mazungumzo baada ya serikali
mpya kuingia madarakani, kwa kuwa kabla ya utekelezaji, imetoa uamuzi wa
kuvunja uhusiano na Tanzania katika MCC.
“Kitu
kinachoitwa demokrasia kingekuwa kinafugwa kwenye bomba na kuona
kinamiminika ingekuwa rahisi sana, lakini ni kitu cha kulea na
kutengeneza. Tanzania imejulikana duniani kama mlezi na mjenzi wa
demokrasia tangu kipindi cha chama kimoja hadi vyama vingi,” alisema.
Aidha,
alisema kutokana na hali hiyo, serikali itafanya marekebisho katika
bajeti yake na mpango wa maendeleo ambao ulijumuisha fedha hizo na
kwamba kinachopaswa kufanyika kwa sasa ni kujikita kwenye ukusanyaji wa
kodi kikamilifu.
“Ndani
ya vikao vya Bunge la Marekani tuna marafiki zetu ambao tunaamini
wataendelea kuihoji serikali yao juu ya uamuzi huu na hasa wakizingatia
historia yetu katika kukuza na kuendeleza demokrasia nchini,” alibainisha.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment