Kufuatia
ubakaji wa demokrasia kupitia kile kilichoitwa uchaguzi wa marudio
uliofanywa juzi tarehe 20 Machi, 2016, jana Mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha, alikamilisha kazi aliyoagizwa
kwa kutangaza kile alichokiita matokeo ya uchaguzi wa Urais.
Chama
Cha Wananchi (CUF) kilishaeleza msimamo wake kuhusu ubakaji huo wa
demokrasia kupitia taarifa yake kiliotoa tarehe 18 Machi, 2016. Baada ya
hatua ya jana tunaweka msimamo wetu kwamba:
1.
Hatutambui hicho kinachoitwa matokeo ya uchaguzi wa marudio wa tarehe
20 Machi, 2016 na kwa maana hiyo hatumtambui huyo aliyedaiwa kuwa
mshindi na kwa msingi huo huo hatutoitambua wala kushirikiana na
Serikali itakayoundwa kutokana na matokeo hayo batili ya uchaguzi
batili.
2.
Tunawapongeza kwa dhati Wazanzibari wote kwa ukomavu wao mkubwa wa
kisiasa waliouonesha kwa kuitikia wito wa mpendwa wao Maalim Seif Sharif
Hamad na chama chao cha CUF na kutoshiriki katika uchaguzi huo batili.
Kwa ujasiri wao huo wameudhihirishia ulimwengu kwa njia za amani na za
kistaarabu kwamba chaguo lao ni Maalim Seif Sharif Hamad. Kwa mara
nyengine tena Wazanzibari wameyathibitisha maamuzi yao ya kidemokrasia
waliyoyafanya kupitia uchaguzi huru na wa haki wa tarehe 25 Oktoba,
2015.
3.
Tunavipongeza vyombo vya habari vya ndani na nje na jumuiya ya
kimataifa kwa kuonesha hali halisi ilivyokuwa na jinsi Wazanzibari
walivyoikataa CCM, walivyowakataa watawala na walivyokataa kutumika
kubaka demokrasia. Wazanzibari wameandika historia nyengine mbele ya
macho ya ulimwengu. Kwa mara nyengine tena Wazanzibari wameshinda.
4.
Tunajua Wazanzibari wana hamu ya kujua hatua zinazofuata katika
kusimamia maamuzi yao ya kidemokrasia waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba,
2015. Chama chao kinawatoa wasiwasi Wazanzibari kwamba hakijayumba na
kinafuatilia haki yao hiyo kwa njia za amani na za kidemokrasia na
kitakuwa kikiwaeleza kila kinachoendelea.
HAKI SAWA KWA WOTE
NASSOR AHMED MAZRUI
NAIBU KATIBU MKUU – CUF
22 Machi 2016
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment