UKATILI WA KUTISHA! Mume Amuua Mke Wake Pamoja Na Mtoto Kwa Kuwachinja Na Kisu Wilayani Bagamoyo Mkoa Wa Pwani

JESHI la Polisi mkoani Pwani linamshikilia Frowin Peter Mbwale (26) mkazi wa Kawe Jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kuua kwa kuwachinja mkewe Oliver Erasto (23) na mtoto wake Emanuel Frowin (3) kutokana na wivu wa mapenzi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa kwa waandishi wa habari Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Bonaventura Mushongi alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa 10:30 usiku eneo la Zinga kata ya Dunda Tarafa ya Mwambao wilayani Bagamoyo.

Mushongi alisema kuwa katika hali isiyo kuwa ya kawaida juzi siku ya tukio mtuhumiwa akiwa na mwenzake alijulikana kwa jina la Rajabu Juma (20) Mkazi wa Makongo Jijini Dar es Salaam waliwaua watu hao kwenye vichaka vilivyopo kwenye eneo hilo la Kaole.

“Muda huo mtuhumiwa akiwa na mwenzake alimhadaa mke wake kuwa waende kwenye nyumba yao ambayo inaendelea kujengwa kwa lengo la kuitazama ambapo mke wake alikubali na kumbeba na mtoto wao na kwenda huko ambako aliwachinja shingoni,” alisema Kamanda Mushongi.

Alisema kuwa mtuhumiwa kumbe lengo lake halikuwa kuangalia ujenzi wa nyumba yao huko Kaole kumbe alikuwa na lengo lingine la kufanya unyama huo ambao aliutekeleza akiwa na rafiki yake huyo ambaye walishirikiana kumchinja mke na mtoto wake.
“Chanzo cha mauaji hayo ni mtuhumiwa huyo alikuwa akimtuhumu mke wake kuwa ana uhusiano na mwanaume mwingine aitwaye Hamza mkazi wa Kawe Jijini Dar es Salaam na kusababisha mauaji hayo ya kusikitisha ambayo yamewaumiza watu wengi,” alisema Mushongi.

Alibainisha kuwa miili ya marehemu hao ilikutwa ikiwa imechinjwa na watu hao umbali wa mita 100 kutoka barabara ya magari itokayo Kaole kwenda eneo la Mbegani.

Aidha alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa majira ya saa 3:30 usiku baada ya wananchi Zinga kuwatilia mashaka walipokuwa wakijaribu kutaka kutoroka na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika, miili ya marehemu imehifadhiwa kwenye Hospitali ya wilaya ya Bagamoyo kusubiri ndugu kwa ajili ya mazishi.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment