Rais MAGUFULI Ashiriki Ibada Ya Kumbukumbu Ya Miaka 32 Ya Kifo Cha Sokoine

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameungana na wakristo wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Joseph Jijini Dar es salaam, kusali misa Takatifu ya kumkumbuka na kumuombea aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Edward  Moringe Sokine aliyefariki dunia miaka 32 iliyopita, kwa ajali ya gari katika eneo la Dakawa wakati akitokea Bungeni Dodoma.

Misa hiyo imehudhuriwa pia na Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Rais Mstaafu wa awamu ya Tatu Mheshimiwa Benjamin William Mkapa na Familia ya Hayati Edward Moringe Sokoine.

Akizungumzia baada ya misa hiyo Rais Magufuli amesema anamkumbuka Hayati Edward Moringe Sokoine, kuwa alikuwa kiongozi shupavu aliyewapenda watanzania, aliyependa kuwatumikia watanzania, aliyekuwa Mchapakazi, aliyechukia rushwa, aliyechukia ufisadi na aliyechukia uonevu kwa watu wa chini.

 "Namuona ni kilelezo cha pekee katika Taifa letu la Tanzania, miaka 32 iliyopita wakati Mzee wetu Hayati Edward Moringe Sokine alipoitwa na kutangulia mbele za haki, wakati huo mimi nilikuwa JKT Mpwapwa, ninaikumbuka siku hiyo ilikuwa ya majonzi makubwa"  Amesema Rais Magufuli.

Hata hivyo Rais Magufuli amesema kazi nzuri ya mtu huwa haipotei na hivyo amewasihi watanzania kuendelea kushikamana, kupendana na kuyaenzi mazuri yote yaliyofanywa na viongozi wa Taifa waliotangulia mbele za haki, wakiwemo hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Hayati Abeid Amani Karume na Hayati Edward Moringe Sokoine.

Kwa upande wake Rais Mstaafu wa awamu ya Tatu Mheshimiwa Benjamin William Mkapa amemuelezea Hayati Sokoine kuwa ni Kiongozi aliyejitoa kutumikia Taifa, na kubainisha kuwa viongozi wote wanawajibika kuishi kwa mfano wake.

Rais Mstaafu Mkapa amesisitiza kuwa mfano huo wa Hayati Sokoine, ndio ulioiwezesha Tanzania kumpata kiongozi wa Sasa, Rais John Pombe Magufuli anayetaka kuonesha misingi ya uongozi bora, uadilifu, kusimamia amani, utulivu na maendeleo.

Nae Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema Hayati Sokoine hakuwa kiongozi wa kujiangalia yeye, bali Kiongozi kwa ajili ya watu, na amempongeza Rais Magufuli kwa kufuata nyayo za Hayati Sokoine katika kuliongoza Taifa.

"Kuna baadhi ya watu wanasema Rais wetu wa sasa ni sura ya Edward Moringe Sokoine" Amesema Kardinali Pengo, na kumtaka Rais Magufuli na serikali yake kusonga mbele na kujenga heshima ya nchi.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
12 Aprili, 2016
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment