WAZIRI
Mkuu, Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa duka la dawa
katika Hospitali Wilaya ya Ruangwa, ambalo litatoa fursa kwa wilaya
nyingine kama Kilwa, Nachingwea na Liwale kufuata dawa katika duka hilo.
Ujenzi
wa duka hilo la dawa ndani ya wilaya ya Ruangwa umefadhiliwa na Bohari
Kuu ya Dawa nchini (MSD) na unakadiriwa kugharimu Sh milioni 55 mpaka
kukamilika kwake.
Litasaidia kuboresha upatikanaji wa dawa hospitalini hapo na katika hospitali zingine zilizoko katika wilaya za jirani.
Majaliwa
alisema mbali na ujenzi wa duka la dawa pia hospitali hiyo inatarajiwa
kujengewa uzio ili kuepusha vitendo vya uhalifu vinavyoweza kutokea
kutokana na kutokuwa nao.
Alisema
hayo wakati akizungumza na watumishi wa hospitali ya wilaya ya Ruangwa
mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa duka la dawa katika
hospitali hiyo.
“Nataka
hapa ndio iwe bohari ya dawa, watu kutoka Kilwa, Nachingwea na Liwale
wawe wanafuata dawa na vifaa tiba katika duka la dawa lililoko ndani ya
Hospitali ya wilaya ya Ruangwa, pia kujengwa kwa duka hili kutasaidia
kumaliza tatizo la upungufu wa dawa,” alisema.
Alisema
mkakati uliokuwepo ni kuhakikisha vifaa tiba na dawa vinapatikana
hospitalini hapo ili kuwawezesha wagonjwa kupata huduma bora.
“Kinachomuuma
ni kuona akinamama, akinababa, vijana na wazee wangu wanakwenda
hospitali na kuambiwa vipimo hakuna, hivyo nitahakikisha vifaa tiba
vyote vinapatikana,” alisema.
Kwa
upande wake, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Dk Japhet
Simeo alimshukuru Waziri Mkuu kwa juhudi mbalimbali anazozifanya
ikiwemo kutafuta wafadhili wanaoendelea kusaidia utoaji wa huduma za
afya hospitalini hapa.
“Mpaka
sasa kuna mradi wa ujenzi wa uzio wa hospitali ya wilaya, ujenzi wa
duka la dawa, ukarabati wa majengo na upanuzi wa hospitali na tunamuomba
aendelee kuwashirikisha wadau mbalimbali katika kutatua changamoto ya
upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali yetu ya wilaya,” alisema.
Dk
Simeo alisema kwa kupitia Waziri Mkuu, wameweza kupata vifaa tiba
mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 100 kutoka umoja wa
kampuni unaotengeneza vinywaji baridi nchini ambavyo jana walikabidhiwa
na Meneja wa MSD, Kanda ya Mtwara, Helman Mng’ong’o.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment