Tamko la Serikali Kuhusu Kutatua Kero na Changamoto za Sekta ya Usafirishaji Barabarani Ikiwemo Kuyaondoa Matuta Yote Barabarani

1.0 Mnamo tarehe 09/4/2015 ulifanyika mgomo wa madereva nchini uliohusu malalamiko na kero  mbalimbali  za  madereva.    

    Katika kuzipatia ufumbuzi kero hizi,  tarehe 02/5/2015 aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Peter Kayanza Pinda,  aliunda Kamati ya Kudumu ya Kutatua Kero na Changamoto mbalimbali katika Sekta ya Usafirishaji. 
    Kamati hiyo inaundwa na Wajumbe kutoka  Serikalini, Umoja wa  Madereva na  Vyama vya Madereva, Vyama vya Watumiaji wa Huduma za Usafiri, pamoja na Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji. Kutokana na  vikao vilivyofanywa na  Kamati hiyo kero na changamoto mbalimbali zilibainishwa na kufanyiwa kazi. Baadhi zimefanyiwa kazi na kukamilishwa; nyingine zinaendelea kufanyiwa kazi ili kukamilishwa na nyingine zitaendela kufanyiwa kazi kwa kuwa ni masuala endelevu.
2.0      Kwa kipindi chote cha utekelezaji wa hatua za kutatua kero na changamoto hizo, kumekuwa na utoaji wa taarifa mbalimbali miongoni mwa wadau kuhusu utendaji na hatua zinazochukuliwa na Kamati. Taarifa hizo zimekuwa zikitolewa kinyume na mamlaka na taratibu zilizokubaliwa na Kamati na zimekuwa zikipotosha umma juu ya usahihi wa hatua na hali halisi ilivyo. 
   Utaratibu huo umekuwa ukisababisha madhara mbalimbali ikiwemo matishio ya migomo miongoni mwa madereva, taharuki miongoni mwa watumiaji huduma na hasara mbalimbali kwa kutokuwepo kwa uhakika wa huduma kwa siku husika. 
 
3.0      Tarehe 01 Aprili, 2016 Kamati ilifanya kikao kilichowajumuisha Mhe. Jenista Mhagama (MB), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu; Mhe. Harrison Mwakyembe (MB), Waziri wa Katiba na Sheria; Mhe. Mhandisi Edwin A. Ngonyani (MB), Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi; Mhe. Anthony Peter Mavunde (MB), Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana na Ajira; Mwakilishi wa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Mwakilishi wa Waziri, Wizara ya Mambo ya Ndani.
   Katika kikao hicho, iliazimiwa kuwa Kamati, kwa kushirikisha wawakilishi wa pande zote, itoe taarifa kwa umma juu ya hatua zilizochukuliwa na mwelekeo uliopo.
 
4.0       Hivyo, Kamati inapenda kutoa taarifa kwa  wadau wote wa sekta ya usafirishaji  na wananchi kwa ujumla kwamba, kufuatia hoja za vikao mbalimbali vya Kamati  ya Kudumu na Kamati Ndogo  vilivyofanyika kati tarehe 12/5/2015 na 01/04/2016, hatua zifuatazo zimechukuliwa:
4.1       Kuhusu kuendelea kutumia mizani ya Kibaha ili kupunguza muda unaotumiwa na mabasi katika mizani ya Vigwaza; Serikali ilifunga Mzani wa Kibaha kutokana na sababu za msingi. Hatua za kuimarisha huduma na kuondoa tatizo la msongamano kwenye mzani wa Vigwaza zimechukuliwa. Hivyo, hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
 
4.2       Kuhusu kushughulikia malalamiko ya wadau juu ya matuta ya barabarani; Serikali imeanza taratibu za kuyaboresha matuta ili yasilete madhara na inaangalia uwezekano wa kuyaondoa matuta yote katika barabara kuu na kuweka alama za vivuko (Zebra) kama inavyoelekezwa na Sheria. Utekelezaji unaendelea na hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
 
4.3       Kuhusu kutoa elimu juu ya matumizi ya mizani inayowezesha gari kupimwa katika mwendo; Hoja imezingatiwa; elimu imeshaanza na inaendelea kutolewa kwa njia mbalimbali za mawasiliano kwa umma, ikiwamo mabango yaliyopo eneo la Vigwaza, vipeperushi kwa Madereva, vipindi vya TV na Redio. Hivyo, hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
 
4.4       Kuhusu kuanzisha utaratibu wa kupima magari bila gharama katika eneo la bandarini kabla ya safari ili kuwawezesha wasafirishaji kuzingatia Sheria kwa kutozidisha uzito; Fedha kwa ajili ya kazi hii zimetengwa katika Mwaka wa Fedha 2015/16, Usanifu umekamilika na taratibu za kumpata mkandarasi wa ujenzi zinaendelea. Hivyo, hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
 
4.5       Kuhusu kutoa taarifa ya maandishi kwa umma kuhusu maamuzi ya kutohitaji vibali kwa ajili ya kuondoa magari mabovu na yaliyopata ajali njiani; Maelekezo yametolewa kwa TANROADS ili vibali visihitajike wakati wa hali ya dharura. Iwapo ajali imetokea au gari limeharibika na kufunga barabara, magari husika yaondolewe na kuyaweka mahali ambapo hayataleta usumbufu kwa watumiaji wengine. Hatua baada ya hapo ni lazima zizingatie taratibu na matakwa ya Sheria. Upatikanaji wa vibali hivyo utarahisishwa zaidi baada ya kuzindua utaratibu wa kupata vibali kwa mtandao (e-permit). Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wameagizwa kuleta taarifa ya utekelezaji katika kikao kijacho.
 
4.6       Kuhusu kufanya ukaguzi wa barabara ili kubaini ubovu na mahitaji ya alama katika maeneo mbalimbali na kuyafanyia kazi; Hoja imezingatiwa na kutekelezwa. Ukaguzi unaendelea kufanyika na alama za barabarani zinawekwa sehemu stahili. Hivyo, kwa kuwa utekelezaji wa hoja hii ni endelevu, Kamati imeagiza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi iendelee kutoa taarifa katika kila kikao, kuhusu maeneo yaliyokarabatiwa na yaliyobaki.
 
4.7       Kuhusu wadau kutoa taarifa kuhusu maeneo yanayopaswa kuwa na alama za barabarani; Wadau wamewasilisha taarifa kuhusu mahitaji ya alama za barabarani zinazostahili kwenye maeneo ya Mlima Sekenke, Iguguno Shamba na Mkoa wote wa Singida; na pia kona zote za Iyovi mkoani Morogoro.
 
Utafiti umefanywa na Wizara ya Ujenzi na kubaini kwamba, jumla ya alama 156 za barabarani zinahitajika kwa mkoa wa Singida. Kwa awamu ya kwanza jumla ya alama 80 zimewekwa kwenye maeneo husika. Utekelezaji unaendelea na Wizara hiyo imeelekezwa kutoa taarifa ya maendeleo katika vikao vijavyo.
 
4.8       Kuhusu kukamilisha ubadilishaji wa aina ya malighafi (materials) itumikayo katika kutengeneza alama za barabarani ili kuzuia kuibiwa kwa alama hizo kwa ajili ya chuma chakavu; Hatua za kubadilisha mali ghafi na kuweka alama za zege kulingana na mahitaji ya eneo husika unaendelea. Hatua za utekelezaji wa zoezi hili zimeanza na pia ni endelevu.
 
4.9       Kuhusu kufanya marejeo (review) ya Sheria na Kanuni ili malipo katika mizani yafanywe pia kwa fedha za Kitanzania; Kamati imeagiza TANROADS kwamba, kwa kuwa ukarabati wa barabara zinazoharibiwa kwa kuzidisha uzito hufanyika kwa dola, malipo ya faini yaendelee kufanywa kwa dola kama inavyoelekezwa na Sheria au kwa fedha za kitanzania kwa kuzingatia viwango halisi vya ubadilishaji fedha vinavyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania wakati wa malipo hayo. Hivyo, hoja hii ya kutaka kurekebisha Sheria imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
 
4.10    Kuhusu wamiliki wa daladala na Jeshi la Polisi kukutane ili kujadili na kukubaliana utaratibu wa utakaotumika katika kufanya ukaguzi wa kawaida wa daladala na kuteua maeneo maalum kwa ajili ya kaguzi hizo; Kikao kati ya Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani na Wamiliki wa Daladala na kuwashirikisha pia madereva, kilifanyika tarehe 05/06/2015. Utaratibu umekubalika na maeneo ya kufanyia kaguzi yamebainishwa. Hoja imefungwa, lakini Jeshi la Polisi limeagizwa kuendelea kushirikisha wadau mara kwa mara na kuwasilisha taarifa katika kikao kijacho juu ya utekelezaji wa zoezi la ukaguzi kama ilivyokubaliwa.
 
4.11    Kuhusu kuimarisha usimamizi wa Sheria na matumizi ya ratiba na batli; Maelekezo yametolewa kwa Wakuu wa Usalama Barabarani wa Mikoa (RTO’s) na usimamizi umeimarishwa. Hatua za utekelezaji zinaendelea na hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
 
4.12    Kuhusu kutoa elimu kwa umma kuhusu utoaji wa taarifa za vitendo vya rushwa vinavyohusisha askari wa usalama barabarani; Elimu juu ya kutoa taarifa za rushwa inaendelea kutolewa kupitia vyombo vya habari kama Redio na Televisheni. Vipeperushi kuhusu rushwa vimeandaliwa na kusambazwa. Uelimishaji umma unaendelea kwa kutumia njia mbalimbali za mawasiliano kwa umma. Hatua za utekelezaji ni endelevu na Jeshi la Polisi limeagizwa kuendelea kushirikisha wadau ili kuweka mikakati ya kupata taarifa za vitendo vya rushwa.
 
4.13    Kuhusu kufuatilia kukamilishwa kwa Kanuni zitakazo wezesha malipo ya faini kufanywa kwa njia ya mtandao; Kanuni zimekamilishwa na Mfumo umeanza kutumika kwa majaribio katika mkoa wa Dar es salaam. Hatua za utekelezaji zitaendelea kwa mikoa yote. Jeshi la Polisi limeagizwa kufanya vikao vya ushirikishaji wadau mara kwa mara. Hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
 
4.14 Kuhusu kuainisha masuala yatakayozingatiwa katika ziara ya mafunzo kwa wajumbe wa Kamati katika nchi jirani; Rasimu ya masuala ya kuzingatiwa bado inafanyiwa kazi. Kamati imeagiza Sekretarieti ifuatilie maoni kutoka TATOA na kushirikisha Vyama vingine vya wamiliki. Hatua za utekelezaji ni endelevu.
 
4.15    Kuhusu kushirikiana na Halmashauri ili kuteua vituo kwa ajili ya pikipiki hasa katika mkoa wa Kigoma; SUMATRA imeanza utekelezaji kwa kutuma mtaalam mkoani Kigoma kwa ajili ya kusimamia zoezi la kuainisha vituo vya pikipiki na bajaji katika Manispaa ya Kigoma-Ujiji. Hatua za utekelezaji ni endelevu. Kamati imeagiza utekelezaji uendelee na hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
 
4.16    Kuhusu kufuatilia kukamilishwa kwa Kanuni zinazotenganisha makosa ya madereva na wamiliki zilizowasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali; Ufuatiliaji umefanywa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali; Rasimu ya Kanuni hizo imeboreshwa na kuwasilishwa tena kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua za mwisho kabla ya kutolewa na kuanza kutumika. Kamati imeagiza Kanuni hizo kukamiliswa haraka, taarifa itolewe na mawasilisho yafanywe katika kikao kijacho. Hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
 
4.17    Kuhusu kufanya utafiti wa mahitaji ya huduma za usafirishaji katika njia kuu; Utafiti umefanywa kwa kushirikisha Chama cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA) katika njia za Dar-Mbeya, Dar-Mwanza na Dar-Arusha; na taarifa inakamilishwa. Kamati imeagiza SUMATRA kuwasilisha taarifa ya matokeo ya utafiti katika kikao kijacho. Hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
 
4.18    Kuhusu kufanya utafiti wa mahitaji ya huduma za usafirishaji katika njia zinazohudumiwa na Daladala katika Jiji la Dar es Salaam; Utafiti utafanywa katika robo ya mwisho wa mwaka wa fedha wa 2015/2016. Hatua za utekelezaji zinaendelea na hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
 
4.19    Kuhusu kutoa leseni za usafirishaji kwa maombi mapya kwa ratiba za magari ya kuanzia saa 1.30 asubuhi na kuendelea; Utekelezaji umeanza kwa magari ya abiria yanayoomba leseni kwa mara ya kwanza. Hatua za utekelezaji wa zoezi hili ni endelevu. Kamati imeagiza wadau kuwasilisha hoja mpya katika kikao kijacho, kama zipo, kuhusiana na suala hili. Hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
 
4.20    Kuhusu kuwasilisha mapendekezo kwa mwakilishi wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji juu ya sekta zinazoweza kuendeshwa na wazawa kwa ufanisi ili kuzingatiwa katika mchakato wa kutengeneza Sera ya usafirishaji kwa ajili ya wawekezaji wa ndani (Local Content Policy); Serikali imeanza kulifanyia kazi suala hili kwa pamoja na sekta nyinginezo chini ya uratibu wa OWM-Uwezeshaji. Hatua za utekelezaji ni endelevu. 
 
4.21    Kuhusu kufuatilia matumizi ya pikipiki, bajaji na magari aina ya Probox (michomoko) katika Mikoa ya Iringa na Kigoma; Ufuatiliaji umefanywa na SUMATRA. Vikao vya mashauriano na wadau vinaendelea. Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi imetoa maelekezo juu ya utatuzi wa suala hili. Kamati imeagiza SUMATRA kutoa taarifa kwa umma juu ya hatua zake na kutoa mrejesho katika kikao kijacho juu ya utekelezaji wa maelekezo ya Wizara. Hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
 
4.22    Kuhusu kuanzishwa kwa jukwaa (forum) la wadau wa usafirishaji kwa barabara; SUMATRA inaandaa mpango wa namna ya kuanzisha jukwaa hili katika robo ya mwisho ya mwaka wa fedha 2015/2016. Hatua za utekelezaji zimeanza na zinaendelea.
 
4.23    Kuhusu wadau kushirikishwa katika kuelewa utaratibu wa ukokotoaji nauli kwa mujibu wa Kanuni; Wadau wameshirikishwa katika utafiti wa hali ya mahitaji ya huduma za usafirishaji (occupancy ratio) katika njia kuu za mabasi ya mikoani ambao upo katika hatua za mwisho za kukamilishwa taarifa. Ushirikishwaji zaidi utafanyika kupitia mafunzo ya ukokotoaji yatakayofanyika ndani ya Robo ya Mwisho wa Mwaka wa fedha 2015/2016. Hatua za utekelezaji zitaendelea kwa daladala. 
 
4.24    Kuhusu kuharakisha ununuzi wa mitambo ya TBS ya ukaguzi wa ubora wa matairi na vipuri; Utaratibu wa ununuzi wa mitambo unaendelea na bajeti imetengwa kwa mwaka 2015/2016. Hatua za utekelezaji zimeanza na zinaendelea.
 
4.25    Kuhusu kutoa elimu kwa umma juu ya utambuzi wa bidhaa zisizo na ubora na hatua za kuchukua, hususani kuhusu matairi ya magari na vipuri; TBS imekuwa ikitoa elimu kwa njia mbalimbali za mawasiliano kwa umma. Hatua za utekelezaji zimeanza na zoezi hili ni endelevu. Kamati imeagiza Mkurugenzi wa TBS awasilishe taarifa katika kikao kijacho juu ya hatua na mikakati ya ukaguzi hapa nchini na katika nchi ambazo TBS haina vituo/wakala wake wa ukaguzi na namna ya kuzuia Tanzania kuwa dampo la bidhaa zisizo na viwango.
 
4.26    Kuhusu kushirikisha sekta binafsi ikiwemo TATOA ili kuwekeza katika vifaa vya ukaguzi wa ubora wa matairi na vipuri; Jukumu la ukaguzi wa viwango vya ubora wakati wa uingizaji bidhaa ni la serikali kupitia TBS. Hata hivyo, watumiaji binafsi hawakatazwi kuwekeza katika kufanya uhakiki wa bidhaa zao baada ya uingizaji huo. Hatua za utekelezaji ni endelevu.
 
4.27    Kuhusu agizo la Kamati kuwa tarehe 20 Agosti 2015, Kamati itembelee mizani ya Vigwaza ili kupata hali halisi ya kero zinazolalamikiwa na madereva na kuona namna ya kuzishughulikia; Kamati ilitembelea Mizani ya Vigwaza tarehe 20/08/2015 kama ilivyoagizwa na mapendekezo ya maboresho yalitolewa kupitia vikao vya Kamati. Uboreshaji umefanywa na hali ya huduma za mzani huo inaridhisha. Agizo limetekelezwa na kukamilika; na hivyo hoja inafungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
 
4.28    Kuhusu Sekretariati kutuma taarifa za mialiko ya vikao na kusambaza Muhtasari mapema ili wajumbe waweze kujiandaa na vikao vijavyo; Maagizo yamezingatiwa na kutekelezwa, kulingana na hali halisi inayojitokeza. Usimamizi wa suala hili utaimarishwa. Hoja imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
4.29    Kuhusu Mamlaka husika (EWURA na WMA) kuwasilisha Mada kuhusu changamoto na taratibu za upakiaji, usafirishaji na upakuaji wa mafuta; Mada ziliwasilishwa na maelezo ya kitaalam kutolewa na wawakilishi wa EWURA, WMA na kampuni ya PUMA katika kikao cha Kamati cha tarehe 11 Machi, 2016. 
     
     Kamati imeagiza EWURA na WMA zifanye utafiti na kutoa taarifa ndani ya siku 60 kuhusu kasoro (shoti) zinazolalamikiwa na wadau, hususani nchini Zambia. Wizara husika ziwasilishe taarifa katika kikao kijacho.
4.30 Kuhusu Serikali kutoa ufafanuzi juu ya matumizi ya Mfumo wa Kukata Nukta katika Leseni za Udereva; Ufafanuzi ni kwamba Mfumo wa ukataji nukta katika leseni za udereva bado haujaanza kutumika. Pindi ukiwa tayari taarifa itatolewa kwa umma. 
     Mfumo huo utatumika kwa kila mtu anayeendesha gari kwa sekta zote, ikijumuisha madereva wa magari binafsi. Hivyo, wadau wameombwa kupata uelewa sahihi kupitia ufafanuzi unaotolewa na Jeshi la Polisi mara kwa mara kupitia vyombo vya habari, badala ya taarifa potofu zinazozagaa mitaani. Hatua za utekelezaji wa hoja hii ni endelevu.
 
4.31    Kuhusu kukamilisha marekebisho na kuwasilisha mkataba wa ajira ya madereva ulioboreshwa katika vikao vya Kamati; Mkataba ulioboreshwa umekamilishwa na kuanza kutumika tarehe 01 Julai, 2015. Wadau walipatiwa nakala ya mikataba na vitambulisho ili waanze kutumia katika sehemu zao za kazi. 
     Ukaguzi ulibaini jumla ya mikataba 11, 133 ilitolewa kwa madereva hadi kufikia Desemba, 2015. Hata hivyo, zoezi la ukaguzi wa mikataba lilisitishwa kwa maombi ya wawakilishi wa wafanyakazi kwamba, lisubiri kukamilika kwa majadiliano na muafaka wa viwango vya posho ili vijumuishwe kwenye mikataba hiyo. 
     Hata hivyo, kwa sasa ukaguzi utaendelea kwa mujibu wa Sheria baada ya wadau kuafikiana hivyo. Utekelezaji wa hoja umekamilishwa na imeondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
 
4.31.1  Kuhusu Serikali kutoa tamko la kuweka viwango vya posho kwa madereva; Vikao vya majadiliano ya wadau yamekamilishwa na kuafikiwa kwamba majadiliano juu ya suala la posho kwa madereva yafanywe kwa mujibu wa Sheria. Hivyo, Kamati imeagiza Vyama vya Wafanyakazi vitekeleze wajibu wake kisheria kwa kufanya majadiliano na Vyama vya Waajiri au Mwajiri mmoja mmoja katika maeneo yao ya kazi.
 
Kufanikisha majadiliano hayo, Vyama vya Wafanyakazi ni lazima viandikishe wanachama kwa asilimia zaidi ya hamsini ya wafanyakazi waliopo sehemu ya kazi ili vipate uhalali wa kuwawakilisha katika majadiliano na mwajiri husika. Wafanyakazi nao wajiunge na Vyama kwa mujibu wa Sheria za Kazi na kuzingatia taratibu za kisheria ili waweze kudai haki, kufanya majadiliano na kupata haki ya kushiriki migomo kwa utaratibu halali iwapo hakutakuwa na muafaka.
 
Kwa upande mwingine, Waajiri wameagizwa pia kuzingatia Sheria kwa kuruhusu Vyama vya Wafanyakazi kufanya shughuli zao katika maeneo yao ya kazi na kufanya majadiliano kisheria ili kudumisha mahusiano mema baina yao, kukuza tija na ufanisi.
 
Kamati imeagiza Idara ya Kazi na SUMATRA kuimarisha kaguzi katika kampuni za usafirishaji na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya yeyote atakayekiuka taratibu zilizowekwa juu ya masuala haya; ikiwemo kuchukua hatua dhidi ya waajiri wasiolipa mishahara wafanyakazi wao au wanaolipa chini ya kima cha chini cha kisheria, kuwashtaki wanaoghushi mikataba na kufuta leseni kwa wanaokiuka masharti ya leseni hizo. 
 
Kamati imeagiza pia, Vyama vya Wafanyakazi viwasilishe mbele ya Kamati, orodha ya wamiliki na madereva wanaokiuka Sheria ili mamlaka husika ziwachukulie hatua stahiki. Majina hayo yatolewe kwa njia za siri kupitia mawasiliano na Afisa Kazi waliyetambulishwa.
 
Hivyo, hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
 
4.32   Kuhusu kuhamasisha madereva kujiunga na Vyama vya Wafanyakazi vilivyopo; Serikali imewezesha kuundwa kwa vyama viwili vya wafanyakazi madereva ambavyo ni Chama cha Wafanyakazi Madereva wa Malori Tanzania (CHAWAMATA) kilichosajiliwa tarehe 28/5/2015 na Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (TADWU) kilichosajiliwa tarehe 25/6/2015.  Uwepo wa Vyama hivyo, pamoja na vile vilivyokuwepo awali, vya TAROTWU na COTWU (T), utawawezesha Madereva kushiriki ipasavyo  katika majadiliano ya pamoja na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji kwa lengo la kuboresha maslahi na haki za madereva.
 
Vyama hivi sasa vinawajibika kisheria kufuata taratibu za majadiliano sehemu za kazi na kuzingatia matakwa ya Sheria na Katiba zao. Vyama husika vimelekezwa kufika katika maeneo ya kazi na kutangaza sera zao kwa njia mbalimbali ili kuvutia wanachama wapya na kuwa na nguvu za kisheria kuwawakilisha na kutetea maslahi ya madereva.
 
Hivyo, hoja hii imekamilishwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
 
4.33      Kuhusu Kutoa mafunzo kwa makundi mbalimbali kuhusu Sheria za Kazi, haki na wajibu wa mfanyakazi na mwajiri; Mafunzo yalitolewa kwa wajumbe wa Kamati, wajumbe wa TATOA na TABOA kwa nyakati tofauti kuanzia tarehe 18 Mei, 2015. Uelimishaji umeendelea kufanywa kwa njia ya vyombo vya habari na ushauri kwa wadau husika kulingana na mahitaji. Utekelezaji ni endelevu na hoja hii inaondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
 
4.34      Kuhusu Serikali kutoa Tamko la kuongeza mishahara ya madareva; Baada ya kupata ufafanuzi wa kisheria, wadau waliafikiana kuwa suala la nyongeza ya mshahara liachwe lishughulikiwe na Bodi za Mshahara kwa mujibu wa Sheria. Uundaji wa Bodi za Mshahara za Kitaifa umeanza na upo katika hatua za mwisho. 
     Bodi hizo ndizo zitakazofanya utafiti kwa mujibu wa Sheria na kuboresha Kima cha Chini cha Mshahara, Vigezo, Hali na Masharti ya Ajira kwa wafanyakazi wa Sekta ya Umma na Binafsi. Madereva wanawakilishwa katika Bodi na watapata fursa ya kutoa maoni yao yafanyiwe kazi huko na kukamilishwa mwanzoni mwa mwaka wa fedha 2016/17.
 
Hivyo, hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
 
4.35      Kuhusu Serikali kufanya marekebisho ya Sheria za Kazi na kuboresha kanuni ili kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa mikataba na maslahi ya madereva; Marekebisho ya Sheria za Kazi, Na. 6 na 7 za mwaka 2004 yalikamilishwa na kupitishwa na Bunge mwezi Julai, 2015. 
      Kanuni za Sheria za Kazi, Na. 6 na 7 za mwaka 2004 nazo zimeboreshwa na zinatarajiwa kukamilishwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kabla ya kutiwa saini na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya kazi na ajira hivi karibuni. Aidha, hatua zinaendelea kufanya marekebisho mapya katika Sheria za Kazi ili kuongeza nguvu za Maafisa Kazi kutoa adhabu za papo kwa papo kwa wakiukaji. 
    Jambo hili litasaidia kutolewa kwa mikataba ya ajira na uzingatiaji Sheria na taratibu za kutoa haki nyingine kwa wafanyakazi wote wakiwemo madereva. Uwezekano unaangaliwa ili adhabu za papo kwa papo ziweze pia kutolewa kwa wafanyakazi watakaobainika kutishia au kuitisha migomo kinyume cha Sheria. 
 
Hivyo, hoja hii imefungwa na kuondolewa mbele ya Kamati kwa sasa.
 
5.0         Hitimisho:
Serikali inatoa wito kwa  wamiliki wa vyombo vya usafirishaji, viongozi wa vyama vya wafanyakazi madereva na madereva wote nchini kuzingatia na kutekeleza makubaliano yaliyokwishafikiwa hadi sasa.

Pamoja na juhudi za Serikali kutatua mgogoro wa ajira ya madereva nchini, kumekuwepo matishio ya mara kwa mara ya kuitishwa migomo kwa madereva. Kamati inawakumbusha Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Madereva na Madereva wote kuzingatia taratibu za kisheria katika kufanya migomo mahali pa kazi, kama zilivyoainishwa katika Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Na. 6 ya mwaka 2004. Kufanya migomo kinyume cha utaratibu ni kuvunja Sheria na hatua stahiki zitachukuliwa kwa wale wote watakaoitisha na kushiriki katika migomo hiyo.
 
Aidha, Serikali itaendelea kutoa elimu na  kufuatilia makubaliano yaliyofikiwa na hatua za kisheria zitaanza kuchulikwa dhidi ya wale watakaokiuka utekelezaji wa makubaliano hayo na matakwa ya Sheria kwa ujumla. Taarifa kwa umma zitaendelea kutolewa juu ya hatua za utekelezaji.
IMETOLEWA NA:
Eric F. Shitindi
     MWENYEKITI WA KAMATI
04/04/2016
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment