Auawa Kwa Kuchomwa Visu Akituhumiwa Kutoka Kimapenzi na Mtalaka Wake

Mkazi wa Kijiji cha Chala B, Tarafa ya Chala wilayani Nkasi, Mkoa wa Rukwa, Moses Nambasita (48) ameuawa kwa kuchomwa visu kutokana na kinachodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Akisimulia mkasa huo mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Vincent Mwanambuu alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 10 jioni baada ya kuvamiwa na kijana mmoja alipokuwa akitoka nyumbani kwake kwenda nyumba jirani, alishambuliwa kwa kuchomwa visu.

Mwanambuu alisema baada ya kupata taarifa hizo alitoa taarifa Kituo kidogo cha Polisi Chala, askari walifika na kuchukua mwili kwa ajili ya uchunguzi na kuanza msako dhidi ya mtuhumiwa.

Akielezea chanzo cha mauaji hayo, Mwanambuu alisema mtuhumiwa alipata taarifa kuwa Nambasita ana uhusiano na mtalaka wake, ambaye walikuwa wameachana kipindi kirefu.

Alidai kuwa kutokana na taarifa hizo, mtuhumiwa alipeleka shauri la ugoni katika Mahakama ya Mwanzo Chala.
“Lakini kabla hata shauri hilo halijamalizika, tunashangaa kuona mtuhumiwa ameamua kujichukulia sheria mikononi, baada ya kutekeleza unyama huo alikimbia na kutokomea kusikojulikana,” alisema.

Mtendaji wa Kijiji cha Chala, Godfrey Mwanakatwe alisema kutokana na mazingira hayo polisi wanawashikilia watu wanne kwa kosa la kushiriki mauaji hayo.

Hatua hiyo inatokana na baada ya wao kutoa taarifa kwa muuaji kuwa Nambasita ana uhusiano wa kimapenzi na mtalaka wake, ambaye mpaka sasa haijulikani alipo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba, baada ya uchunguzi wa polisi ndugu wa marehemu waliruhusiwa kuuzika mwili huo.

Mwaruanda alisema chanzo cha kifo hicho ni wivu wa mapenzi na kuongeza kuwa mtuhumiwa alianza vizuri kwa kufuata sheria, lakini haijulikani kilichosababisha kuchukua uamuzi huo wa kinyama.

Alisema wanawashikilia watu watatu wakituhumiwa kushiriki mauaji hayo, kwa kutoa taarifa kwa mtuhumiwa kwamba Nambasita alikuwa na uhusiano na mtalaka wake.
Kamanda Mwaruanda aliwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi, hivyo wafuate taratibu kupata haki zao.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment