Shirika la Kimataifa la Polisi linawasaka raia wawili wa Scotland
wanaodaiwa kukimbilia Tanzania baada ya kufanya udanganyifu na kujipatia
Paundi 20 milioni za Uingereza (sawa na Sh62 bilioni).
Wawili hao,
Gareth Johnson (48) na Geoffrey Johnson (72) walikuwa sehemu ya kundi la
watu 18, lililohusishwa na uhalifu huo wa uchakachuaji ongezeko la kodi
ya simu za mkononi nchini Uingereza.
Kutokana na kosa hilo,
Mahakama Maalumu ya Mapato na Forodha ya Uingereza (HMRC) iliamuru
wanafamilia hao, ambao ni baba na mwanae, walipe fidia ya Paundi 109
milioni (sawa na Sh337 bilioni).
Lakini hukumu hiyo ilitoka bila
ya wawili hao kuwapo baada ya kutoroka kabla ya shauri hilo kuanza
kusikilizwa na inasemekana walikimbilia Tanzania.
Akizumgumzia suala
hilo, Mkuu wa Interpol Tanzania, Gustavus Babile alisema kibali cha
kimataifa cha kukamatwa kwa wawili hao kipo kwenye tovuti yao.
Alisema
walipokea taarifa kutoka Uingereza hivyo hatua inayofuata ni kukipeleka
kibali hicho mahakamani kwa ajili kupata nguvu za kisheria za nchi.
Balile
alisema baada ya hatua hiyo, utafanyika uchunguzi ili kubaini kama
watuhumiwa hao wapo nchini. “Kama wapo watakamatwa,” alisema.
Picha
na majina ya raia hao wa Scotland zimebandikwa kwenye tovuti ya
Interpol kwa kuwekewa bendera nyekundu, ikiwa ni alama ya kusakwa na
polisi hao wa kimataifa.
Awali, alipoulizwa kuhusu hilo, msemaji
wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba alisema litashughulikiwa baada ya
Uingereza kutoa taarifa ya watuhumiwa hao.
Hadi sasa inadaiwa kuwa Geoffrey na kijana wake
wamekuwa “mafichoni” Tanzania kwa takriban miaka mitatu sasa.
Mapema
Aprili mwaka huu, Gazeti The Mirror la Uingereza liliripoti kuwa wawili
hao, ambao wametakiwa kulipa fedha hizo mara moja au waongezewe adhabu
ya kifungo cha miaka 14 jela, wamebainika kuwapo nchini.
Kwa
mujibu wa gazeti hilo, uchunguzi wa awali ulibaini kuwa makazi yao mara
baada ya kufika nchini yalikuwa jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, wakati uchuguzi huo ukibaini hilo, mienendo yao inaonyesha kuwa kwa sasa wapo mkoani Iringa.
Inadaiwa
kuwa Geoffrey, ambaye Mahakama iliamuru afungwe jela miaka 10 katika
hukumu ya mwaka 2014, ni wamiliki wa kampuni ya Johnson International
Group ambayo makazi yake ni Kipawa jijini Dar.
Kampuni ya
Johnson, ambayo inasimamiwa na kijana wake ambaye pia alihukumiwa
kifungo cha miaka 10 jela, imeajiri wafanyakazi 125.
Lakini,
taarifa ya gazeti hilo kwenye mtandao wake, inaeleza kuwa kampuni hiyo
haina uhusiano mzuri na wafanyakazi wake kwa sababu haijawalipa mshahara
kwa muda mrefu.
Kutokana na mvutano uliokuwapo kati wa wafanyakazi hao
na waajiri wao, wafanyakazi 40 walipeleka madai yao kwa mkuu wa mkoa
mwaka 2014.
Pia, wafanyakazi hao walidai kunyanyaswa hasa pale
walipoomba kuongezwa mshahara huku mwajiri wao akiwatishia kuondoa
michango yao ya pensheni.
Mmoja wa wasimamizi wa kampuni ya
Johnson, Leonard Lukule alisema hali hiyo imesababishwa na hali mbaya ya
kiuchumi ndani ya kampuni.
“…Kuna wakati tulilazimika kutoa likizo za lazima kwa wafanyakazi,” alisema Lukule.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment