Hayo yamebainishwa na Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Bw. Rhoben Nkhori wakati wa Mkutano wa Mashauriano wa CRB uliofanyika jijini Dar es Salaam na kufunguliwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Bw. Nkhori amesema kuwa katika jukumu la kuratibu mwenendo wa kazi za makandarasi, Bodi ilikagua miradi 2735. Katika miradi hiyo iliyokaguliwa, miradi 1873 sawa na asilimia 68.5 haikuwa na kasoro.
Ameongeza kuwa miradi mingine ilikuwa na kasoro za kutofanywa na makandarasi waliosajiliwa, kutozingatia usalama wa wafanyakazi, kutokuwa na bango wala uzio na miradi kutosajiliwa. Kwa mujibu wa Bw. Nkhori miradi yote iliyopatikana na upungufu wahusika walichukuliwa hatua mbali mbali kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Bwana Nkhori amesema kuwa kwa mwaka jana, Bodi ilisajili miradi 3,172 yenye thamani ya shilingi trilioni4.23. Katika miradi hii asilimia 44.4 ilifanywa na Makandarasi wazawa na asilimia 55.6 ilifanywa na makandarasi wa kigeni.
Licha ya mafanikio hayo CRD ilikumbana changamoto kadhaa ikiwemo kuwasilisha nyaraka za kugushi wakati wa usajili hususani kadi za magari na mitambo, vyeti vya wataalam, kutumia majina ya makandarasi kwa udanganyifu kwa kuuza vibao, waendelezaji kutotoa taarifa sahihi za umiliki kwa Bodi na baadhi ya makandarasi kushindwa kuwalipa wafanyakazi na vifaa vya ujenzi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi, Bi Consolata Ngimbwa amemwomba Mhe. Rais John Pombe Magufuli kuwapa kipaumbele Makandarasi wa humu nchini ili kuwawezesha kiuchumi. “Mhe. Rais tunaomba utupe kipaumbele kwani sisi tukipata hiyo miradi tutawekeza hapa nchi na kuongeza soko la ajira,”alisema Bi Ngimbwa.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema serikali yake itawapa kipaumbele makandarasi wazawa lakini akawataka wajipange na kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia maadili ikiwemo kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Mkutano huu pamoja na mamabo mengine utajadili jinsi ya kuwajengea uwezo makandarasi nchini. Kauli mbiu ya Mkutano huo ni “Juhudi za Makusudi za kukuza uwezo wa makandarasi wazawa, changamoto na mustakhabali.”
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment