Sakata la uuzwaji kinyemela wa zaidi ya hekari 200 za shamba la Umoja wa
Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Iringa limechukua sura
mpya baada ya aliyekuwa katibu wa mkoa huo, Ally Nyawenga kukamatwa na
polisi.
Shamba hilo lililopo eneo la Igumbiro, nje kidogo ya mji
wa Iringa, linadaiwa kuuzwa mwaka jana kwa zaidi ya Sh800 milioni baada
ya baadhi ya viongozi kubadili matumizi yake na kuwa viwanja.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, John Kauga alisema jana kuwa kiongozi huyo alikamatwa Morogoro siku chache zilizopita.
“Tulituma
askari wetu na leo hii wanamleta. Taarifa za kumkamata ni hizo za
uuzwaji wa shamba hilo kwa hivyo tutafanya naye mahojiano zaidi, lakini
kwa sasa sina taarifa zaidi ya hapo labda tuwasiliane kesho (leo),”
alisema.
Nyawenga alisimamishwa kazi mwishoni mwa mwaka jana,
akituhumiwa kusimamia uuzwaji wa shamba hilo kinyume cha utaratibu wa
jumuiya hiyo.
Mali zote za jumuiya hiyo zipo chini ya Baraza la
Wadhamini, linaloongozwa na Mwenyekiti, Dk Emmanuel Nchimbi.
UVCCM
ilianza kumiliki shamba hilo miaka ya 1970 likitumika kwa ajili ya
kilimo kwa kukodisha vijana kwa bei nafuu ili kuwasaidia kujiendeleza
kiuchumi.
Ally Simba aliyedaiwa kuwa msimamizi wa shamba hilo alikana nafasi hiyo huku akisema hakuhusishwa katika mipango hiyo.
“Sikuwa
msimamizi, bali mjumbe tu wa kamati ya utekelezaji, msimamizi alikuwa
Katibu wa UVCCM,” alisema Simba ambaye kwa sasa ni Katibu wa UVCCM
Wilaya ya Mbinga.
Alisema kabla ya kuondoka Iringa mwaka 2014, hakuwahi kusikia vikao wala mipango ya uuzaji wa shamba hilo na kwamba hahusiki.
Akizungumzia
kukamatwa kwa Nyawenga, Katibu wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Abdulkarim
Halamga alisema: “Kwa sababu ni mali ya vijana na katibu aliyekuwapo
anahusika, hivyo kwa kushirikiana na polisi, tumemkamata baada ya
waliouziwa viwanja kuanza kutudai huku vijana wakipinga kuuzwa kwa eneo
lao. Kwa sababu hakuwa peke yake, taratibu nyingine zitafuatwa
akishafikishwa Iringa.”
Mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya UVCCM
mkoani hapo, Thom Muyinga alisema kuuzwa kwa shamba hilo kumesababisha
mpasuko ndani ya umoja huo. “Vijana wanataka mali yao, haiwezekani mali
hiyo iuzwe kinyemela na kunufaisha kundi la watu wachache,” alisema.
Mmoja
wa vijana hao, Katula Kalinga alisema japo tayari tume ya UVCCM ya
kuchunguza mgogoro huo ilishakwenda Iringa, hakuna kinachoendelea.
Alimuomba Rais John Magufuli kufuta hati za viwanja hivyo ili shamba hilo, lirejeshwe kwa UVCCM.
Pia,
walimuomba Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete kutumbua majipu
yanayokitafuna chama kwenye mkoa huo, ili vijana waendelee kunufaika na
mali yao.
Walitaka kamati ya utekelezaji jumuiya hiyo Mkoa wa Iringa isimamishwe wakati uchunguzi ukiendelea.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment