MBUNGE
wa Viti Maalumu, Angelina Malembeka (CCM) ametaka watu wanaohukumiwa
kifungo cha maisha jela kwa kosa la ubakaji na ulawiti, wahasiwe ili
wawapo gerezani wasiendeleze tabia hizo.
“Tumeshaona
wanaohukumiwa kifungo cha maisha, wakiwa huko gerezani wanaendeleza
vitendo vya kulawitiana, kwa nini sasa wasihasiwe?” Alihoji.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe, wakati akimjibu jana alisema, “siwezi
kuwa na jibu kwa sababu Bunge ndilo linalotunga sheria, mbunge aje na
wazo lake hapa bungeni lipitishwe kama sheria sisi Serikali hatuwezi.”
Akitoa
ufafanuzi zaidi juu ya hali ya ubakaji na ulawiti, Dk Mwakyembe alisema
kila siku nchini kunaripotiwa matukio 19 ya kubakwa na kulawitiwa.
Alisema
hali ni mbaya sana na sasa kuna mashauri 2,031 yaliyoripotiwa
mahakamani katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu.
Kati
yake mashauri hayo, 111 yameshakamilishwa kwa kuhukumiwa ambapo watu 99
wamefungwa, watuhumiwa 18 wameachiwa huru kwa kukosa ushahidi na kesi
1,920 hazijakamilika.
Akijibu
swali la msingi la mbunge huyo aliyehoji mpango wa Serikali kuhakikisha
kesi za kubakwa na kulawitiwa hazimalizwi kifamilia, Dk Mwakyembe
alisema kumalizwa kwa kesi kifamilia kunachochea vitendo hivyo kuendelea
katika jamii.
“Tatizo
la kuficha ushahidi na kumaliza kesi hizo kifamilia, haliwezi kumalizwa
na vyombo vya dola peke yake bila ushirikiano na wananchi wanaoishi na
watuhumiwa. Hivyo Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa umma kuwa kuficha
ushahidi na kuyamaliza matukio hayo ya jinai kifamilia si kosa peke
yake, bali vilevile utaratibu huo unachochea vitendo hivyo kuendelea
katika jamii,” alifafanua.
Ili
kuweka mazingira rafiki kwa waathirika na wananchi wenye taarifa au
ushahidi wa aina hiyo, alisema Serikali imeanzisha madawati ya jinsia
katika vituo mbalimbali vya Polisi yanayopokea taarifa mbalimbali kutoka
kwa wananchi na kuliwezesha Jeshi la Polisi kuendesha upelelezi kwa
ufanisi.
“Pindi
tukio la kubaka au kulawiti litakaporipotiwa, upelelezi hufanyika na
mtuhumiwa kufunguliwa mashitaka mara moja, kwa utaratibu huu Serikali
inahakikisha kuwa matukio haya hayamalizwi nje ya utaratibu wa haki
jinai,” alisema.
Sheria
ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 imeweka adhabu ya kifungo cha maisha kwa
mtu yeyote anayekutwa na hatia ya kumbaka msichana. Pia sheria imeweka
adhabu ya kifungo cha miaka 14 kwa kosa la kulawiti.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment