Kamati ya Bunge Yaingilia Kati Madaktari Kutumbuliwa Majipu

Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imelaani wanasiasa wanaoingilia utendaji katika Sekta ya Afya kwa kutoa adhabu kwa madaktari na wauguzi, bila kushirikisha vyombo vyao.

Wakizungumza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jana, wajumbe hao waliitaka Serikali kuepuka unyanyasaji dhidi ya madaktari na wauguzi ili kurudisha amani iliyokuwapo katika sekta hiyo.

Kamati hiyo ilimbana kwa maswali Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamis Kigwangalla ambaye alijitetea hajahusika kusimamisha madaktari na wauguzi tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Peter Serukamba alipongeza hatua ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kuingilia kati suala hilo kwa kutoa tamko la Serikali.

Alisema analaani pia Watanzania wote ambao wanachukua sheria mkononi na kuwaadhibu madaktari, akisema tabia hiyo haifai kuvumiliwa.
“Madaktari na wauguzi wana chombo chao. Kama wamekosea tuwapeleke kwenye vyombo vyao watapewa onyo au kuchukuliwa hatua za kinidhamu, jamani tuache siasa kwenye Sekta ya Afya,” alisema Serukamba.

Alisema watoa huduma ya afya wana umuhimu mkubwa katika jamii, lakini siku za hivi karibuni wameonekana kunyooshewa vidole kwa kila jambo wanalolifanya na kuifanya sekta hiyo yenye watumishi wachache kukosa molari.

Akijibu hoja hiyo, Dk Kigwangalla alisema katika kulinda hadhi ya madaktari suala la wananchi kujichukulia sheria mikononi limeikera sana Wizara ya Afya.

Alisema wananchi wamepewa fursa ya kutoa maoni yao katika kila hospitali na kituo cha huduma za afya, hivyo wanapaswa kutoa malalamiko yao na kama watahitaji usiri wafunge katika bahasha maalumu.
“Nitumie nafasi hii kuwataka wananchi wafuate taratibu kadri zilivyowekwa kwa mujibu wa sheria kufikisha malalamiko yao,” alisema Dk Kigwangalla.

Kamati hiyo ilihoji sababu za jengo la Taasisi ya Mifupa (MOI) kuanza kutumika kabla ya ujenzi kukamilika.
Dk Kigwangalla, baada ya kubanwa na kamati hiyo iliyosema kuna mgogoro kati ya mkandarasi anayejenga na taasisi hiyo, aliuagiza uongozi wa MOI kumpa taarifa sahihi kuhusu mkandarasi huyo.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment