Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella Aamuru Kurudiwa Kwa Uhakiki wa Watumishi HEWA Mkoa wa Mwanza

Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella, ameagiza kurudiwa upya kwa zoezi la uhakiki la kuabaini watumishi hewa katika mkoa wa Mwanza, ikiwa ni mpango wa kubaini wale wote wanao lipwa mishahara bila kufanya kazi, zoezi hilo litafatia zoezi lililofanyika awali ambapo mkoa huo ulibainika kuwa na watumishi hewa wapatao 334.

Mongella amesema pamoja na kumalizika kwa zoezi la awamu ya kwanza la kuhakikiwa kwa watumishi hewa na kubainika watumishi wapatao 334 tumeamua kufanya upya zoezi hilo ili kuwa na idadi kamili ya watumishi wanaolipwa fedha za serikali bila kuzifanyia kazi.

Amesema tayari taratibu zinachukuliwa ikiwa ni pamoja kuunda jopo la kuhakiki kutoka ngazi ya mkoa kwenda kwenye halmashauri zote za mkoa huo kwa ajili yakufanya uhakiki upya wakiwa na Payroll.

“Nimesha muagiza Katibu Tawala wa Mkoa, kuwa, Wakurugenzi wote kufika kesho( leo) saa 6.00 kamili mchana yaani tarehe 05.04.2016 (Pay roll) zote ziwe zimewasilishwa mezani kwake, ili wataalam kutoka ngazi ya mkoa waweze kwenda nazo wilayani kwa ajili yakufanya uhakiki upya” alisema Mongella na kuongeza:

”Tunataka kwenda kufanya uhakiki wa mtu kwa mtu (physical), popote pale walipo warudi wahakikiwe labda kama yupo masomoni nje ya nchi."

Ameagiza wale wote walioko masomoni, likizo au safari warudi mara moja kwenye vituo vyao vya kazi kwa ajili ya zoezi la uhakiki, huku akiwataka wote watakao kwenda kwa ajili ya kuhakikiwa waende wakiwa na picha tatu za passport size, ambapo taratibu zakuweka kumbukumbu sahihi zitafanyika

“Tunataka zoezi hili lichukue muda wa siku saba tu na baada ya hapo tutatoa ripoti kamili, tusishangae kuona idadi hiyo ikiongezeka au kupungua kwani katika uhakiki huu naamini tutapata majibu sahihi " alisema Mongella.

Aidha alisema hata kuwa na mzaha na yeyote atakayebainika kulea matatizo ya watumishi hewa katika mkoa huo, hivyo lazima kila mmoja awajibike kwa nafasi yake aliyo ajiriwa nayo. 

Katika hatua nyingine Mongella, amevitaka vyombo vya habari katika mkoa huo kumpatia ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake ya ulinzi na usalama, kusimamia maendeleo na kujua ustawi wa watu wa Mwanza

 “Mwandishi wa habari hatofautiani na kachero wa Polisi, sasa tusaidiane kuongoza huu mkoa kwakupeana taarifa, maana mkoa huu ni mkubwa, sio rahisi kwa Mkuu wa mkoa kujua yote yanayoendelea hadi ngazi ya kijiji lakini kwakuwa ninyi wenzangu mnao wigo huo basi tusaidiane ili watu katika mkoa huu waweze kufanya kazi zao kwa amani na salama." Alisema Mkuu huyo wa Mkoa wa Mwanza. 
Imetolewa na: Atley J. Kuni 
AFISA HABARI NA UHUSIANO 
OFISI YA MKUU WA MKOA WA MWANZA 
04.April,2016
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment