WENJE wa CHADEMA Aiomba Mahakama Imkubalie Vielelezo Vyake

Wakili anaemtetea Ezekiah Wenje katika kesi ya kupinga ubunge wa Jimbo la Nyamagana, Deya Outa, amewasilisha ombi dogo Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, akiomba fomu ya uchaguzi namba 21B zitumike kama ushahidi wao.

Kesi hiyo imefunguliwa na Wenje (Chadema) akipinga ushindi wa Mbunge wa jimbo hilo, Stanslaus Mabula (CCM) kupitia uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.

Akiwasilisha ombi hilo mahakamani hapo mbele ya Jaji Kakusulo Sambo wa mahakama hiyo jana, wakili Outa aliiomba mahakama iangalie jitihada zilizofanywa na mteja wake (Wenje), kuhakikisha kesi yake inasikilizwa, pia jitihada alizofanya za kukusanya fomu hizo na kuziambatanisha kama kielelezo na kuwaleta mashahidi wa fomu 646.

Alidai wajibu maombi (Mabula na wenzake wawili) wanafahamu mleta maombi anahitaji kuzitumia fomu hizo, pia walipewa taarifa mapema katika hatua za awali za uainishaji wa vielelezo vya ushahidi.

Upande huo uliwasilisha ombi hilo mahakamani hapo chini ya kifungu 13(4) cha Sheria ya Uchaguzi Sura ya 447 ya mwaka 2010, kifungu cha 13 cha mwenendo wa makosa ya madai, ukiomba kutolewa kwa fomu hizo mashahidi waweze kuzitolea ushahidi.

Hata hivyo, upande wa wajibu maombi ukiongozwa na Wakili Mwandamizi, Constatine Mutalemwa, pamoja na upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Vincent Tangoh, uliomba muda wa siku mbili kupitia kumbukumbu za mahakama pamoja na rekodi za kesi hiyo kwa ufasaha zaidi ili wajipange na kujiandaa kujibu maombi hayo.

Mahakama ilikubali ombi la kuongezewa muda kwa upande wa wajibu maombi na upande wa Jamhuri ili uweze kujipanga na Jaji Sambo aliamuru upande wa wajibu maombi kwenda na majibu leo saa 3:00 asubuhi wakati kesi hiyo itakapoendelea kusikilizwa.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment