Akizungumza ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema mauaji hayo yalitokea Mei 31, mwaka huu saa 4.10 usiku katika Mtaa wa Ilemela katikati ya barabara inayopita kati ya eneo zilipo ofisini za Radio Free Afrika (RFA) na Kiwanda cha Samaki cha Mwanza.
Alisema polisi waliokuwa doria katika eneo hilo waliwatilia mashaka watu watatu waliokutana nao usiku huo wakiwa wamebeba sanduku na walipoamriwa kusimama, hawakutii.
“Hawakutii, badala yake watu wale waliongeza mwendo, huku mmoja wao akitoa mfuko uliokuwa na kitu, kumbe ilikuwa ni bunduki na kuanza kurushiana risasi na polisi,” alieleza Kamanda Msangi.
Alisema mtu huyo alifyatua risasi kati ya tatu hadi nne kwa polisi, lakini hazikuleta madhara kwa walinzi hao wa usalama wa raia waliomuua kujibu mapigo kwa kumpiga risasi na kumuua papo hapo huku wenzake wawili wakikimbia na kuelekea kusikojulikana.
Alisema baada ya tukio hilo, polisi walimkuta jambazi huyo akiwa na silaha aina ya SMG iliyochakaa na namba zake zikiwa zimefutika ikiwa na magazini yenye risasi 16. Alisema upelelezi kwa ajili ya tukio hilo unaendelea.
Kamanda Msangi alisema silaha iliyokamatwa hutumika kwenye majeshi na kuwa mwananchi wa kawaida haruhusiwi kutumia silaha ya aina hiyo.
“Tutapeleka silaha hii kwa wataalamu kwa ajili ya kuitambua maana bunduki ya aina hii hatuna kwenye majeshi yetu,” alisema na kuongeza kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa ajili ya utambuzi.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment