KIKWETE: Nchi za Afrika Haziwezi Kukwepa Misaada ya Wazungu


Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amesema nchi za Afrika haziwezi kukwepa misaada kutoka nchi za Ulaya kwa kuwa misaada hiyo ni jukumu lao la kihistoria.

Kikwete alisema hayo jana wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku mbili unaojadili malengo mapya 17 ya Umoja wa Mataifa yanayohusu ‘Maendeleo Endelevu kwa mwaka 2030’.

Mkutano huo umejikita kujadili lengo namba 16 linalohimiza haki, amani na jamii shirikishi, hasa katika masuala ya utawala wa sheria kama chachu ya maendeleo endelevu.

Kikwete alisema jukumu hilo linapaswa kuendelezwa kwa kuwa maendeleo ya nchi za Ulaya yalitokana na rasilimali walizozitoa Afrika kipindi cha ukoloni.

Alisema nchi za Afrika zina rasilimali za kutosha hivyo, ili zifanye kazi bado kunahitajika uwekezaji ambao utaweza kuinua viwanda na kukuza uchumi wa nchi za Afrika, kwani bila hivyo itachukua muda mrefu kufika mbali kiuchumi.

Hata hivyo, alisema nchi za Afrika lazima zijiwekee utaratibu wa namna ya kupokea misaada hiyo, lakini lengo liwe ni kunufaisha wazawa na kwa kufuata sheria za nchi husika na zile za kimataifa.

“Misaada tunayoizungumzia siyo lazima iwe fedha, bali tunahitaji wawekeze zaidi kwetu kwa mikataba ya kisheria inayolinda wazawa, kwa mfano Tanzania tuna rasilimali za kutosha kama gesi, madini na vinginevyo, lakini hivi vyote vinahitaji kuibuliwa na kutayarishwa. Lazima tuwape nafasi ili kufanikisha lakini kwa sheria zitakazowalinda Watanzania,” alisema Kikwete.

Kauli hiyo ya Kikwete imekuja wakati Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli amekwisha kuweka msimamo katika hotuba zake kadhaa akitaka Tanzania ijitegemee kwa asilimia kubwa badala ya kutegemea misaada ya nje.

Wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya kwanza ya juu (flyover) katika makutano ya Barabara za Mandela na Nyerere eneo la Tazara, Rais Magufuli aliita misaada ya wahisani ‘mkate wa masimango’ na kusema kuliko kula mkate huo ni bora kushindia muhogo.

Ingawa hakufafanua wala kuzungumza kwa undani juu ya kauli hiyo, lakini aliitoa ikiwa zimepita siku chache tangu Shirika la Maendeleo la Milenia (MCC) la Mareka ni kusitisha msaada wa Dola za Marekani milioni 472.8 karibu Sh1 trilioni kwa madai kuwa Tanzania ilikiuka misingi ya kidemokrasia kwa kurudia uchaguzi wa Zanzibar na kushindwa kusimamia She ria ya Makosa ya Mtandao.

Pia, Rais Magufuli Machi 29, akiwa katika kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato mkoani Geita alisema jukumu kubwa lililo mbele ya Watanzania kwa sasa ni kushikamana na kujisimamia katika maendeleo ili kila mmoja ahakikishe anaongeza uzalishaji na utendaji kazi mahali pake pa kazi.

“Kwa hiyo ni lazima tujisimamie sisi wenyewe, na tukijisimama sisi wenyewe kwa kila mmoja kuwajibika mahali alipo, kama ni mfanyakazi afanye kazi kwelikweli, kama ni mkulima afanye ukulima wake kwelikweli, kama ni mfanyabiashara afanye biashara kwelikweli, kama ni mfugaji afuge kwelikweli, kama ni mvuvi avue kwelikweli, Tanzania hii tutavuka,” alisema.

Mkutano huo ulioandaliwa na Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo ya Sheria (IDLO) yenye makao makuu yake nchini Italia, ambayo kwa Tanzania mlezi wake ni Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mkapa alisema katika nchi yeyote ili kupata maendeleo ni lazima kuwe na Katiba ya wananchi ambayo haitalenga kundi moja.

“Awali nchi nyingi za Afrika hazikuwa na Katiba ya wananchi, bali kulikuwa na Katiba ya chama ambayo kwa sasa ni nchi za kidikteta pekee zimebaki na mfumo huo, kwa sasa tulilenga kuweka sera, mikakati thabiti ili tuweze kutekeleza malengo mapya ya dunia chini ya dira mpya ya Umoja wa mataifa ya maendeleo ya dunia,” alisema Mkapa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki alisema kama ilivyo ajenda ya nchi za Afrika, nchi haiwezi kuwa na utawala wa sheria kama hakuna upatikanaji mzuri wa sheria.

“Lazima uweke mifumo mizuri ya kutatua migogoro pia, utoaji wa vibali bila kutoa rushwa, hata katika uwekezaji utakapokuwa huna sheria nzuri inayolinda upande huo ni vigumu wawekezaji kuwepo,” alisema Kairuki.

Mkurugenzi Mkuu wa IDLO, Irene Khan alisema mkutano huo umejikita katika kujadili haki, amani na jamii shirikishi.
“Lengo ni kuwa na dira mpya ya maendeleo ya dunia inayolenga kutokomeza umaskini, kulinda mazingira, kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kushirikisha makundi yote kwenye jamii katika masuala ya maendeleo,” alisema Khan.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment