WAZIRI
wa mambo ya ndani ya nchi Mwigulu Nchemba, amesema kuwa Serikali
itahakikisha inakabiliana kwa nguvu zote na tatizo la makazi ya askari
polisi nchini ili kulipa hadhi jeshi hilo ambalo linakabiliwa na
changamoto mbalimbali.
Nchemba aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na maafisa
wa jeshi hilo pamoja na askari wa kawaida wa mkoa wa Dodoma katika kikao
kazi kilichofanyika kwenye bwalo la jeshi hilo mjini Dodoma.
Mwigulu
alisema kuwa mojawapo ya suala ambalo wizara yake italipa kipaumbele ni
makazi ya askari wa jeshi hilo ambayo mengi hivi sasa yamechoka na
kukosa hadhi ya kutumiwa na askari wa jeshi hilo.
“Suala la makazi
tutalipa kipaumbele kikubwa sana na tutaanza hatua kwa hatua kulifanyia
kazi suala hili ili askari wetu waondokana na adha hii wanayoipata kwa
muda mrefu sasa,” alisema Mwigulu.
Alisema kero nyingine
watakayoifanyia kazi ni kuhakikisha kuwa mazingira ya kufanyia kazi kwa
askari polisi yanaboreshwa kuanzia kazini kwao na pia kwenye makazi yao.
“Kumekuwapo na tatizo la mafuta kwa jili ya magari mnayoyatumia … hata tukio likitokea mnashindwa kufika kwa kukosa mafuta.
"Pia
kuna maslahi duni, umeme maofisini pamoja na nyumbani mnapoishi imekuwa
ni kero kubwa kwenu hivyo sisi kama wizara tutahakikisha haya yote
tunayaondoa,” alisema Mwigulu.
Katika hatua nyingine, Mwigulu
alitoa rai kwa askari polisi nchini kuhakikisha kuwa wanazingatia miiko
ya kazi yao kwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili kama ambavyo
walivyofundishwa katika mafunzo yao.
“Mimi uwepo wangu hapa sijaja
kuwafundisha kazi kwakuwa tayari kazi yenu mnaijua… ambayo mmefundishwa
mkiwa chuoni. Hivyo sisi kama wizara jukumu letu ni kuweka mazingira
wezeshi ili mfanye kazi zenu katika mazingira mazuri,” alisema.
Aidha
alilitaka jeshi hilo kutumia nguvu katika mahali panastahili tu kufanya
hivyo ili hata mwanachi akisikia utendaji wao ajivunie uwapo wa jeshi
hilo.
“Tumieni nguvu mahali mbapo Mtanzania wa kawaida akisikia
ajivunie uwapo wenu kama ambavyo mmejitahidi katika suala la madawa ya
kulevya. Kama tutaweza kuubaini mnyororo huo na kuukata, mwanchi wa
kawaida atajivunia,” alisema.
Aidha alisema kuwa jeshi hilo bado
lina kazi kubwa ya kufanya ili kukomesha mtandao wa watu wanaojihusisha
na madawa ya kulevya nchini na pia akalitaka jeshi hilo kuhakikisha
linakuwa mtetezi wa wanyonge.
Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma,
Lazaro Mambosasa, awali akimkaribisha Waziri Mwigulu alisema kuwa jeshi
hilo limejipanga vilivyo katika kuhakisha uhalifu unakomeshwa mkoani
hapa.
“Mweshimiwa waziri mwenye utakuwa ni shahidi ukiwa katika
vikao vya bunge uliona namna ambavyo amani na usalama ulikuwepo wa
kutosha. Hii yote ni kutokana na kujipanga vizuri kwa jeshi la polisi
mkoani hapa,” alisema Mambosasa.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment