UPOTOSHAJI
kuhusu makato ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika miamala ya
benki na simu za mikononi, uliotangazwa na baadhi ya benki, umeilazimu
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoa ufafanuzi na kuzuia benki hizo
kutoza kodi kwa wateja wao.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamishna Mkuu wa TRA,
Alphayo Kidata, alihoji kwa nini mabenki yametoa matangazo ya kuanza
kutoza kodi hiyo, wakati hata kanuni za utekelezaji wa sheria hiyo
hazijatolewa.
Kidata
alisema pamoja na kupitishwa kwa sheria hiyo bungeni, lakini muongozo
unaotokana na kanuni bado haujatolewa, ndio maana TRA imeshindwa kuelewa
kwanini taasisi hizo zimetoa taarifa zao kwa wananchi.
Kutokana
na hali hiyo ya kutoa matangazo ya kutekeleza sheria hiyo, wakati
kanuni za kutekeleza sheria yenyewe hazijatolewa, Kidata alisema
kumeonekana dalili za nia ovu.
“Tangu
lini mmeona benki au taasisi ya fedha inaanza kutoa matangazo ya
utekelezaji wa sheria za serikali? Hii ni kwa sababu ya nia ovu.
“Kuna
taarifa ambazo si za kweli zinazoenezwa kupitia mitandao ya kijamii
kuwa VAT itatozwa kwenye amana ya mwenye fedha kwenye benki. Hii si
kweli,” alisema Kidata.
Usahihi wa kodi
“Juzi
Bunge la Tanzania lilipitisha marekebisho ya sheria hiyo ya mwaka 2014
kuanzia Julai mosi mwaka huu kwenye huduma za kifedha kwa kurekebisha
kifungu cha 13 cha jedwali la msamaha wa kodi, lakini taasisi hizo
zimekuwa zikipotosha umma,” alisema.
Alisema
kutokana na upotoshaji huo, TRA imeamua kueleza ukweli kuhusu
utekelezaji wa sheria hiyo, ili kuondoa utata na upotoshaji unaohusu
utekelezaji wa sheria hiyo.
Kidata
alisema sheria hiyo inalenga kutoza VAT kwa kiwango cha asilimia 18,
kwenye ada ambazo benki zinatoza wateja wake katika huduma mbalimbali
zitolewazo na benki au taasisi za fedha.
“Ukweli
ni kuwa kiasi cha VAT kitakachotozwa ni asilimia 18 ya kiasi cha
gharama ya huduma iliyotolewa na benki au taasisi yoyote ya fedha na si
kwa mteja,” alisema.
Akitolea
mfano suala hilo, Kidata alisema kama ada ya huduma ya benki ambayo
mteja ametozwa ni Sh 1,000, VAT itakayotozwa kwenye kiasi hicho ni Sh
152.50 tu na benki kubaki na Sh 847.50 na si kuwaongezea wananchi mzigo.
“Kiwango
hiki cha Sh 152.50 ndicho kitakachorejeshwa serikalini na benki au
taasisi ya fedha baada ya kupunguza VAT iliyolipwa kwenye manunuzi
ambayo yamefanywa kwa benki au taasisi ya fedha husika. Kwa mujibu wa
sheria hii, VAT haitatozwa kwenye riba inayotozwa na benki kwenye
mikopo,” alisema.
Alisema
kuna maelezo yametolewa na moja ya benki hapa nchini kuwa mtumiaji wa
huduma za kifedha, atatakiwa kulipia kwa fedha taslimu kama muamala
husika haukupitia kwenye akaunti na kuongeza kuwa taarifa hiyo siyo
sahihi, kwa kuwa ukusanyaji wa VAT husika, utafanywa kwa njia ile ile
ambayo gharama za huduma za kifedha zinakusanywa sasa.
Kidata
alisema TRA itatoa maelekezo ya namna utoaji wa risiti za kielektroniki
utakavyofanyika, ili kuwezesha mabenki au taasisi za kifedha kutimiza
matakwa ya kisheria ya VAT ya mwaka 2014 kama ilivyorekebishwa mwaka
2016.
“Hivyo
tunazitaka benki na taasisi za fedha zilizoamua kwa makusudi kutoa
taarifa zisizo sahihi kwa umma, kuacha mara moja vinginevyo hatua kali
za kisheria zitachukuliwa.
“Kimsingi
benki na taasisi za fedha zinazohusika zinaagizwa kurekebisha mara moja
taarifa walizokwishazisambaza ili zibebe maudhui sahihi ya marekebisho
ya sheria hii,” alisema.
Barua BoT
Alisema
katika hatua za awali, tayari wamewapa maelekezo Benki Kuu (BoT) ambayo
ni msimamizi wao mkuu, ihakikishe hicho kinachofanyika kinasitishwa na
hatua mbalimbali za kisheria zitachukuliwa.
“Mwanzo
benki na taasisi hizo za fedha zilikuwa zikichukua tozo yote
wanayotoza, hivyo sasa tumewataka katika hiyo hiyo waliyokuwa
wakichukua, ndiyo watoe kodi na si kumuongezea mwananchi mzigo kwa
sababu kila kodi ina msingi wake na si kila kodi inapopanda, imlenge
mwananchi. Sisi tumelenga hiyo hiyo wanayotoza,” alisema.
Alitoa
mwito kwa mtu yeyote mwenye uhakika kuwa ameongezewa makato na benki au
taasisi za fedha kwa madai ya utekelezaji wa sheria hiyo, atoe taarifa
ili hatua zaidi za kisheria zichukuliwe.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment