Kamanda Tibaigana alitoa kauli hiyo hivi karibuni katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu akisisitiza kuwa kila jambo linalofanyika hapa duniani ni lazima liongozwe kwa Sheria na Kanuni.
Ingawa sheria nyingi za nchi mbalimbali duniani zinafanana lakini kila nchi imejiwekea sheria na kanuni za kufuata katika kufanya jambo lolote au katika kutafuta suluhu ya migogoro mbalimbali ikiwemo ya kisiasa, kidini, kijamii pamoja na ya kiuchumi.
Tanzania ni nchi mojawapo inayoongozwa kwa Sheria na Kanuni mbalimbali na ndio sababu hata katika Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa nchi imeeleza wazi kuwa hakuna aliye juu ya sheria wala hakuna anayeruhusiwa kuzivunja sheria hizo.
Anasema kuwa ili Taifa litengemae ni lazima wananchi wafuate Sheria na Kanuni zilizowekwa kwa sababu kutofuata sheria ni kosa kubwa.
Tibaigana anaongeza kuwa Sheria ni msumeno, ni vema kila pande ikaheshimu sheria na kanuni hasa kwa kutambua madaraka ya kila mmoja yanaanzia wapi na yanaishia wapi ili kuzuia tatizo la muingiliano wa majukumu ambao unaweza kusababisha uvunjifu wa sheria na kanuni zilizowekwa na nchi husika.
Aidha, Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeelezea kwa undani pamoja na kuweka sheria na kanuni zinazohusu maandamano ya aina yoyote ,yawe ya kisiasa, kidini, kijamii au ya kiuchumi.
“Sheria inamtaka mwananchi au kundi la wananchi wanaohitaji kufanya maandamano kutoa taarifa kwa maandishi kwa Mkuu wa Polisi wa eneo husika kabla ya masaa 48 ya kuanza kwa maandamano hayo ikieleza dhumuni la maandamano hayo, pia wahusika wanatakiwa wawe tayari kwa jibu lolote kutoka kwa mkuu huyo kwa kuwa chochote watakachojibiwa lazima kiwe na sababu”, anasema Tibaigana.
Tibaigana anafafanua kuwa kama wahusika watakataliwa kufanya maandamano na hawatoridhishwa na sababu zilizotolewa na Mkuu wa Polisi kuna hatua mbili muhimu zinazotakiwa zifuatwe na sio wahusika kujiamulia kuandamana kilazima kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa.
Hatua hizo muhimu zinazotakiwa kufuatwa ni kuandika barua kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na kumueleza kuwa hawajaridhika na sababu zilizotolewa na Mkuu wa Polisi ili waziri naye kwa upande wake aamue kuruhusu au kukataza, endapo wahusika hawatoridhika na majibu ya waziri, watatakiwa kwenda Mahakamani ambapo ndipo uamuzi wa mwisho utatolewa.
Anasisitiza kuwa hakuna sheria inayotambua maandamano ya nchi nzima kufanyika kwa siku moja kwa sababu kila eneo lina Mkuu wa Polisi mwenye haki ya kukubali au kukataa ombi la kufanya maandamano kulingana na hali halisi ya eneo lake.
Kila jambo lina faida na hasara zake lakini kuna mambo ambayo faida huwa chache kuliko hasara, maandamano yana athari kubwa kiuchumi na kijamii kwa sababu maandamano yoyote ni lazima Jeshi la Polisi liwajibike katika kuongoza na kulinda maandamano hayo, hivyo kupelekea wanajeshi wengi kusitisha kazi zingine kwa ajili ya kuzuia vurugu zisitokee.
Athari zingine ni kusitishwa kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za usafiri , kufungwa kwa maduka na masoko pamoja na athari zitokanazo na vurugu zinazoweza kutokea kwa sababu ya maandamano hayo.
Aidha, Kamanda Tibaigana anatoa ushauri kwa vyama vya siasa vinavyotumia maandamano kama njia ya kupata usuluhishi wa migogoro yao kufata sheria na kanuni zilizowekwa kwani maandamano mengi ya aina hiyo yanasababishwa na kutaka nafasi ya kuongoza nchi kwahiyo kama chama hakitoheshimu sheria za nchi lazima kiwe mfano mbaya kwa wananchi watakaowaongoza.
Watanzania wanatakiwa kuelewa kuwa maandamano sio njia pekee ya kusuluhisha migogoro yao bali njia bora ni kukaa chini na kuelewana kwa njia ya mazungumzo, huo ndio utamaduni wa nchi yetu kwani hali hiyo ya kutii sheria na kanuni umepelekea nchi kuendelea kuwa na amani wakati wote.
“Sisi ndio walinzi wa amani hiyo kwahiyo yatupasa kuzitii sheria zetu ili kuitunza amani yetu daima”.
-Credit: Jacquiline Mrisho – MAELEZO
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment