Awali, mawakili wa NHC walidai kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo na kwamba mkataba baina ya Mbowe na NHC juu ya umiliki wa jengo la Bilcanas lililopo mtaa wa Makunganya jijini Dar es Salaam umeisha.
Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Peter kibatala ulidai kuwa, mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, hivyo inaweza ikatoa uamuzi wowote na ndiyo maana wamewasilisha maombi hayo ili yatolewe uamuzi.
Akitoa uamuzi wa pingamizi la mawakili wa NHC, baada ya kuwa amesikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili, Jaji Siyovelwa Mwangasi amesema kuwa hoja za Mawakili wa NHC hazina mashiko kisheria kwani suala la mkataba wa umiliki Jengo hilo linahitaji ushahidi.
Jaji Mwangasi amesisitiza kuwa zuio la NHC kutopiga mnada mali za Mbowe, lilizozichukua wiki mbili zilizopita kupitia mawakala wa kampuni ya Fosters Auctioneers katika ukumbi wa Bilcanas na katika ofisi za kampuni ya Free Media upo pale pele.
Shirika hilo linamtuhumu Mbowe kutolipa deni la Sh. 1.3 bilioni, ikiwa ni jumla ya fedha za kodi ya kupangishwa kwenye jengo hilo huku Mbowe akifungua kesi katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi, kupinga madai hayo ya NHC.
Katika kesi hiyo namba 722 ya mwaka 2016, Mbowe anawakilishwa na Mawakili na Peter Kibatala na Omary Msemo ilihali NHC ikiwakilishwa na mawakili wake Aloyce Sekule na Miriam Mungula.
Katika hoja zake Mbowe anadai kuwa, yeye na shirika hilo walikubaliana kwamba alikarabati na kulipanua jengo hilo kwa gharama zake kwa asilimia 100, makubaliano ambayo waliyaingia mwaka 1997.
Katika makubaliano hayo, Mbowe amedai kuwa walikubaliana kumiliki jengo hilo kwa pamoja kwa muda wa miaka 99, huku yeye akitakiwa kupata asilimia 75 katika mgawanyo wa mapato na NHC ikitakiwa kupata asilimia 25.
Hivyo amedai kuwa hatua ya NHC kumtoa kwenye jengo na kuchukua mali zake ni kuvunja mkataba huo. Mbowe aliondolewa kwenye jengo hilo mnamo Septemba Mosi mwaka huu.
Baada ya mahakama kufanyia uamuzi pingamizi lililowekwa na mawakili wa NHC, kesi hiyo imeahirishwa mpaka tarehe 27 Septemba, mwaka huu ambapo itaanza kusikilizwa rasmi.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment