Wakunga
wanaokiuka maadili ya kazi ikiwemo kuwatolea wajawazito maneno ya
kashfa na kejeli, wametangaziwa ‘kiama’ baada ya serikali kuagiza Baraza
la Wakunga kuhakikisha wanaobainika, wanafutiwa leseni.
Aidha,
serikali imeamua kuanzia mwaka ujao wa fedha, halmashauri zote
zitapaswa kuorodhesha idadi ya watakaopoteza maisha wakati wa kujifungua
sanjari na sababu za vifo na kama upo uzembe, ifahamike mtu wa
kumwajibisha.
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
alisema hayo jana kwenye maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani
yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Alisema
ingawa wapo wakunga wengi wazuri na waadilifu, wapo wachache wasio
waadilifu ambao amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais
John Magufuli haitawavumilia.
“Ukweli
ni kuwa wakunga wengi ni wazuri na waadilifu, kwani wanafanya kazi
katika mazingira yenye changamoto nyingi. Lakini wapo wachache ambao
siyo waadilifu, … wakumbusheni wanachama wenu maadili ya kazi zao mara
kwa mara, ” alisisitizia Baraza la Wakunga.
Katika
maadhimisho hayo yenye kaulimbiu ya ‘Wanawake na watoto mhimili wa
wakunga’, Waziri alisema ili kuwawajibisha wakunga wenye tabia hizo, ni
vyema wananchi wanaofanyiwa ukatili kuwataja wahusika moja kwa moja
badala ya kuunganisha wakunga wote kwenye kituo husika.
Alisema katika masomo ya ukunga, wanataaluma hao wanafundishwa jinsi ya kuhudumia mjamzito. “Anayeona hawezi kazi hiyo ni vyema kuacha na kutafuta kazi nyingine,” alisema.
Alisema
serikali haitamwonea huruma yeyote atakayesababisha vifo kwa
wajawazito. Alisema watapitia halmashauri zote kuangalia zilivyotenga
bajeti kwa ajili ya kukabili vifo hivyo.
Alifafanua
kuwa pamoja na wakunga kukabiliwa na mzigo mzito wa kufanya kazi katika
mazingira magumu ya ukosefu wa vitendea kazi, kuhudumia wajawazito
wengi kuliko viwango vinavyotakiwa, hiyo si sababu ya kufanya vitendo
hivyo vya ukatili kwa wajawazito.
Waziri
alikiri wanataaluma hao kukabiliwa na changamoto kwa kusema, kwa sasa
mkunga mmoja anahudumia wajawazito kati ya 10 na 80 wakati viwango vya
kawaida inapaswa mkunga mmoja kuhudumia mjamzito mmoja hadi sita.
Hata
hivyo alisema, kuanzia mwaka ujao wa fedha, serikali itaongeza idadi ya
wanafunzi wanaojiunga kusomea masuala ya ukunga ikiwa ni pamoja na
kuongeza ajira kwa wakunga serikalini.
Marekebisho elimu ya ukunga
Akizungumzia
ubora wa elimu kwa wakunga, alisema wameanza kufanyia marekebisho kwani
baadhi ya mambo yanatokea kutokana na kutoa elimu kwa muda mfupi wa
miaka miwili tofauti na ilivyokuwa awali miaka minne.
“Hivyo
tumeanza kuboresha utoaji wa elimu kwa kushirikiana na Baraza la
Wakunga na tayari imefika Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE)
ambapo majadiliano yanaendelea na watakapokamilisha, suala la mishahara
nalo litaangaliwa kwa watakaosoma miaka mingi tofauti na sasa,” alisema.
Awali Mkurugenzi wa Chama cha Wakunga Tanzania (Tama), Feddy Mwanga alisema kwa sasa wana matawi 23 na wanachama 4,000 .
Alisema
serikali itakapowekeza kwa wakunga kwa kuwapa utaalamu wa stadi zote
zinazotakiwa watapunguza vifo vya wanaojifungua kwa asilimia 70.
Alisema
mkunga akipata utaalamu huo ana uwezo wa kumhudumia mjamzito kwa
asilimia 87 na zinazobaki ni kwa wachache wanaotakiwa kufanyiwa
upasuaji.
“Hivyo
tunaona ni vyema kuangalia upya elimu ya uuguzi na ukunga iliyopunguzwa
kutoka miaka minne hadi miwili kwani muda hautoshi kumtengeneza mkunga
ipasavyo,”alisisitiza.
Alisema
Tama inasikitishwa na tabia ya wakunga wachache wanaokiuka maadili kwa
kutoa huduma isiyostahili. Alisema wataendelea kuwachukulia hatua
watakaobainika.
Hata
hivyo, akizungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo lawama
na tuhuma kwa wakunga, alisema wakati mwingine hutokana na uelewa mdogo
wa huduma za afya ya uzazi.
Alitoa
mfano wa tukio la hivi karibuni lililoripotiwa kwenye baadhi ya vyombo
vya habari; ambalo mjamzito alilalamika kutupiwa mtoto kifuani baada ya
kujifungua, alisema haikuwa unyanyasaji bali ni suala la kitaalamu.
“Tunaomba
wananchi watutie moyo kwa kazi nzito tunayofanya na wasitupige pale
kunapotokea tatizo kwani wakati mwingine ni kutokana na uelewa wa kazi
yetu kama ilivyokuwa kwa mama aliyewekwa mtoto kifuani,” alisema.
Alikiri
kwamba bado hawajaelimisha kuhusu suala hilo la kuweka kifuani mtoto
anayezaliwa kwa ajili ya kumpatia joto jambo ambalo lilitafsiriwa na
mama huyo kuwa ni unyanyasaji
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment