Waziri Mkuu MAJALIWA Awatembelea Waathirika Wa Mafuriko Iringa, Apokea Misaada Ya Maafa Ya Sh. Milioni 86/-


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea misaada mbalimbali yenye thamani ya sh. milioni 85.88/- kwa ajili ya wananchi walioathirika na mafuriko kwenye vijiji vya kata ya Mlenge, tarafa ya Pawaga, wilaya ya Iringa vijijini mkoa wa Iringa.

Misaada hiyo imetolewa na wadau mbalimbali kutokana na mafuriko ambayo yalibomoa nyumba 82 katika kitongoji cha Kilala, kijiji cha Kisanga na kuwaacha wananchi wake bila makazi.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kasanga ambako alikwenda kukagua athari za mafuriko na kuwapa pole wananchi hao jana mchana (Jumatatu, Februari 22, 2016), Waziri Mkuu aliwashukuru wadau wote waliojitolea kuwachangia watu waliopata maafa kutokana na mafuriko hayo.

Wadau waliotoa misaada hiyo ni Benki ya NMB mabati 500, mifuko ya saruji 500, kilo 820 za maharage, kilo 750 za unga wa mahindi na lita 250 za mafuta ya kupikia vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni 20/-. Wengine ni Mfuko wa Pensheni wa PPF uliotoa mabati 200 na mifuko ya saruji 200 vyenye thamani ya sh. milioni 6.6/-.

Wengine ni Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) waliotoa mabati 200 na mifuko ya saruji 160 vyenye thamani ya sh. milioni 4.5/-; Kiwanda cha kusindika nyanya cha RedGold kimetoa mifuko ya saruji 100 na mabati 50 vyenye thamani ya sh. Milioni 3/-; mbunge wa viti maalum kwa tiketi ya CHADEMA, Bi. Susan Chogisasa na wenzake wametoa mabati 150, mifuko 23 ya saruji, kilo 100 za maharage, kilo 50 za chumvi na nguo mbalimbali vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni 1.3/-.

Madiwani wa Iringa Vijijini walitoa sh. 380,000/-, Wabunge wa Viti Maalum kupitia CCM walitoa vifaa vya sh. Milioni 1.7/-; ofisi ya CCM Mkoa wametoa vifaa vya sh. milioni 6.1/-, Kamanda wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Bw. Salim Abri aliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Iringa sh. milioni 5/- ili wanunue vyakula vya waliopatwa na maafa.

Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni mbunge wa Isimani, Bw. William Lukuvi alitoa fedha taslim sh. milioni 20/- kati ya hizo sh. milioni 15 zikiwa ni zake na milioni 5/- ni za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Bw. George Simbachawene. Pia alikabidhi seti 251 za mashuka zenye thamani ya sh. milioni 4/- zikiwa ni mchango kutoka Benki ya CRDB.


Waziri Lukuvi ambaye alishatoa mabati 250, aliahidi kuongeza mabati mengine 250 (yote yana thamani ya sh. milioni 8), pia alikabidhi sh. milioni 1.5/- kwa diwani wa Mlenge ili ziwasaidie kukodi gari la kukarabati barabara yao ambayo imeharibika sana kutokana na mafuriko hayo.

Mapema, akitoa taarifa ya maafa kwa Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bi. Amina Masenza alisema jumla ya kaya 82 zilikosa makazi kutokana na mvua zilizonyesha Februari 12 na kusababisha mafuriko. Kabla ya hapo, kaya nyingine 75 zenye wakazi 377ziliathirika kutokana na mvua zilizoanza Februari 3, mwaka huu.

Alisema miundombinu ya barabara na ya maji safi iliharibiwa vibaya na kusababisha hasara ya zaidi ya sh, milioni 250/-. Pia wakazi hao walikumbwa na ugonjwa wa kipindupindu kutokana na mto Mapogoro kufurika na kusomba baadhi ya vyoo vya wakazi hao.

“Tangu Februari mosi, wamekwishapokea wagonjwa wa kipindupinda 351 lakini walioko wodini hivi sasa ni wagonjwa 25 tu,“ alisema Mkuu huyo wa mkoa.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, FEBRUARI 22, 2016.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwapa pole wanawake na watoto wakati alipotembelea makazi ya dharura waliyojengewa na serikali katika kijiji cha Kasanga wanapohifadhiwa waathirika wa mafuriko yaliyozikumba tarafa za Pawaga na Idodi , Iringa Februari 22, 2016.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea taarifa ya msaada kutoka kwa meneja uhusiano wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Lulu Mangele katika mkutano wa kuwapa pole wananchi wa tarafa za Pawaga na Idodi uliohutubiwa na Waziri Mkuu katika Kijiji cha Kasanga, Iringa Februari 22, 2016. Mfuko huo umetoa mabati 200 na saruji mifuko 200 vyote vikiwa na thamani ya sh. 6,600,000/=.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwapa pole kinamama na watoto wakati alipotembelea makazi ya dharura waliyojengewa na serikali katika kijiji cha Kasanga wanapohifadhiwa waathirika wa mafuriko yaliyozikumba tarafa za Pawaga na Idodi , Iringa Februari 22, 2016.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment