AGIZO LA RAIS MAGUFULI NA MUSEVENI LAANZA KUTEKELEZWA

UTEKELEZAJI wa agizo la marais wa Tanzania, Dk John Magufuli na Uganda, Yoweri Museveni; kutaka kasi katika ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda kupitia Kaskazini mwa Tanzania hadi Bandari ya Tanga, umeanza na imeshaainishwa kuwa litapita katika mikoa saba.
Taarifa , zimeeleza kuwa Alhamisi wiki hii, serikali za Tanzania na Uganda pamoja na kampuni ya Total E&P Uganda na Shirika la Maendeleo ya Petroli la Tanzania (TPDC), wametia saini mpango wa pamoja wa utekelezaji wa mradi huo.

 Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mpango huo umetiwa saini na Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, Profesa Sospeter Muhongo; Waziri wa Maendeleo ya Nishati na Madini wa Uganda, Irene Muloni; Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk James Mataragio na Meneja Mkuu wa Total E&P Uganda, Adewale Fayemi.
Kuhusu maeneo bomba hilo litakapopita, taarifa hiyo imeeleza kuwa bomba hilo litaingia nchini kupitia Mkoa wa Kagera na kuingia mikoa ya Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma hadi bandari ya Tanga.

 Mpango huo umesainiwa ikiwa ni wiki mbili tangu Rais Magufuli na Rais Museveni kutoa tamko la pamoja la utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba hilo. Hivi karibuni Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total Afrika Mashariki, Javier Rielo, alimhakikishia Rais Magufuli, kuwa kampuni hiyo itaanza ujenzi wa bomba hilo haraka iwezekanavyo, kwa kuwa fedha za kutekeleza mradi huo zipo.

 Katika mazungumzo hayo, Rielo alimueleza Rais Magufuli kuwa kampuni yake inatarajia kutumia dola za Marekani bilioni 4 ambazo tayari zimeshaandaliwa. Bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1,410 na litasafirisha mafuta ghafi mapipa 200,000 kwa siku kutoka Ziwa Albert nchini Uganda, hadi Bandari ya Tanga na ujenzi wake unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment