Kocha Mkuu wa Azam, Muingereza, Stewart Hall.
Omary Mdose, Dar es Salaam KOCHA Mkuu wa Azam, Muingereza, Stewart Hall, ameshindwa kuiweka timu yake katika orodha ya timu zinazowania ubingwa wa Ligi Kuu Bara, akidai Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), tayari linamjua bingwa wa ligi hiyo.
Hall ameyasema hayo kutokana na kile anachoamini kwamba waamuzi wa michezo ya ligi kuu kwa kushirikiana na TFF wamekuwa wakiwanyonga, hivyo hata kama wakipambana itakuwa ni kazi bure tu.
Azam kwa sasa inashika nafasi ya tatu katika ligi ikiwa na pointi 50, sawa na Yanga, huku Simba ikijikita kileleni kwa pointi 57, lakini imewapita wanaowafuata kwa michezo mitatu.
“Katika ligi tupo nafasi ya tatu lakini tuna uwezo wa kutoka nafasi hii na kwenda juu kutokana na kuwa na michezo mitatu mkononi, siwezi kusema tunaweza kuwa mabingwa msimu huu wakati kuna watu tayari wameshamuandaa bingwa wao, kawaulize TFF watakwambia bingwa wa msimu huu ni nani,” alisema Hall.
Mara kwa mara, Hall amekuwa akiwatupia lawama TFF kwa jinsi waamuzi wanavyochangia matokeo mabaya kwao huku akitolea mfano kwamba wameweza kuwa mabingwa wa Kombe la Kagame na kuwafunga Bidvest Wits mchezo wa awali wa Kombe la Shirikisho Afrika nyumbani kwao kwa mabao 3-0, hiyo yote ni kwa sababu waamuzi hawakuwa na upendeleo kwa yeyote.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment