WAZIRI MUHONGO AWATAKA WAMILIKI WA MIGODI KULIPA USHURU HADHARANI

SERIKALI imeagiza ulipaji wa ushuru wa huduma unayofanywa na migodi mbalimbali nchini ufanyike hadharani ili kila mwananchi aelewe kiasi kilicholipwa.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alitoa agizo hilo hivi karibuni alipofanya ziara kwenye mgodi wa dhahabu wa Cata Mining uliopo katika kijiji cha Kataryo, mkoani Mara ambako alikagua shughuli za mgodi huo na kuweka jiwe la msingi.muhongo

Profesa Muhongo alisema ili kuondoa hali ya sintofahamu pamoja na kuongeza uwazi na utekelezaji sahihi wa miradi kutokana na fedha zitokanazo na malipo ya ushuru wa huduma, ni lazima ulipaji huo wa ushuru husika ukashuhudiwa na kila mwananchi.

Waziri Muhongo alimuagiza Kamishna wa Madini kuandika barua kuikumbusha migodi yote nchini pamoja na halmashauri ambazo kuna migodi kufuata utaratibu uliowekwa. “Migodi itaandaa mfano wa hundi ya malipo husika na italipa hadharani kwenye mikutano ya hadhara ili kila mwananchi wa eneo husika ashuhudie, na aelewe kiasi halisi kilicholipwa,” alisema.

Aidha aliongeza:“Asilimia 0.3 inayolipwa kama ushuru wa huduma ni lazima iende kwenye miradi ya maendeleo ya maeneo husika na sio vinginevyo, ” alisisitiza.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment