SEHEMU YA 7: Meja Jenerali MSUYA; Alivyokufa na Kufufuka

ILIPOISHIA:
Yeye alinifanyia utafiti wa uvimbe mbalimbali niliokuwa nao na akaamua kuuondoa mmoja uliokuwa chini ya mfupa wa shingo (mtulinga) ambako hapakuwa na hatari ya kukata mshipa wa fahamu. Aliniambia kurejea siku ya tarehe 19. Niliporejea alinipa dawa za ganzi na kuung’oa uvimbe huo akampatia mtaalam wa magonjwa kwa ajili ya uchunguzi.
ENDELEA…

Jumatatu ya tarehe 25 matokeo yakaonesha kwamba uvimbe huo ulikuwa unaitwa Lymphomas, Diffuse B-Cell Nonhodgekins Lympoma ambayo ni aina ya kansa mbaya ya tezi za limfu (lymph) ambayo tayari ilikuwa imefikia hatua ya nne kutokana na kutogundulika mapema.

Kutoka hapo Dk. Sheaves alinielekeza kwa mtaalam wa masuala ya damu (hematology) ambaye angechunguza aina ya matibabu ambayo yangetibu ugonjwa huo. Kwa bahati mbaya, siwezi kulikumbuka jina la mtaalam huyo (jina lake lilikuwa kama Profesa Praddock, lakini sina uhakika), lakini kabla ya kutoa dawa za kutibu kansa, alinielekeza kwa mmoja wa wasaidizi wake, jamaa mmoja wa Nigeria, kufanya uchunguzi iwapo kansa ilikuwa imeathiri uboho wa mifupa au uti wa mgongo.

Kwa kweli, Mnigeria huyo alikuwa makini. Aliingiza sindano kwenye mfupa wa kwenye kalio ili kupata uboho na akatumia pia sindano ili kupata maji ya mgongoni na akaniambia nirejea siku iliyofuata ili kulazwa.
Nilirejea eneo la 22 Devonshire Place tarehe 24 ambako nililazwa. Matokeo yalionesha hapakuwa na seli zozote zenye kansa katika uboho au uti wa mgongo; hata hivyo, waliamua kwamba wangeweka kiasi kidogo cha dawa katika uti wa mgongo kwa kupitia sindano.

Walifanya hivyo, tarehe 27. Siku ya tarehe 28 dozi nzima ya dawa ilitumika kwa saa ishirini na nne. Niliendelea kuwa chini ya uangalizi kwa siku kadhaa na kuruhusiwa kuondoka Jumamosi, tarehe 30.
Mwanetu, Bis, alituchukua kutoka hotelini hapo na sote tulikwenda na kuondoka katika ile hoteli tukaelekea Birmingham, nyumbani kwake. Wikiendi hiyo ilipita bila tukio lolote hadi tukaingia mwezi Agosti kwa furaha, tukichanganyikana na wajukuu zangu, Catherine, Reece, Keir na Maiya. (Hadi sasa tumebarikiwa kuwa na wajukuu saba. Wengine watatu ni: Ronald, Samuel Jr na Anabelle).

Hiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kumwona Maiya kwa vile alikuwa na umri wa miezi 11 tu; lakini siku mbili alitushangaza kwa kuniita kwa Kiswahili, ‘Babu’. Hii ilitokana na kuwasikia kaka zake wakiniita ‘Babu’.
Wataalam wa mambo ya damu jijini London walitupa muda hadi Jumatatu tarehe 8 kurejea kwa ajili ya kutathmini na kupanga miadi kwa ajili ya duru lililofuata la dawa; hata hivyo, ilipofika Ijumaa tarehe 5 Agosti, nilianza kujisikia vibaya. Ilipofika saa mbili nilizimia. Kutoka wakati huo na kuendelea, ninachoandika ni simulizi kutoka kwa mke wangu na mwanangu.

Mwanangu aliita gari la wagonjwa ili linikimbize hospitali. Madaktari wa eneo hilo walileta gari dogo ambalo lilishindwa kunibeba nikiwa nimekaa kwenye kitu cha magurudumu; hivyo waliita gari kubwa kutoka kwenye kituo chao cha dharura. Mwanangu anaishi mwendo wa dakika 15 kutoka Birmingham Heartland Hospital ambako ilibidi nikimbizwe.


Mkuu wa matabibu hayo aliniuliza nilivyokuwa najisikia. Nilijibu nikisema kwamba nilikuwa niko salama. Alinitazama na kusema ‘huonekani kama uko salama’; kisha walinibeba kutoka kitandani na kuniweka kwenye kiti cha magurudumu. Chumba changu cha kulala kilikuwa ghorofa ya kwanza, hivyo walipata tabu kidogo kuniteremsha chini.
Baada ya kuniingiza katika gari la wagonjwa, mkuu wao alinidunga sindano moja, bila shaka ili kuimarisha utendaji kazi wa moyo wangu; kisha alimwamuru dereva aondoke.

Gari liliondoka kwa kasi na kuingia mitaani huku king’ora kikilia kutoa onyo kwa waendesha magari wengine kwamba kulikuwa na mgonjwa aliyetakiwa kupewa huduma haraka, hivyo ilibidi walipishe gari hilo.
Tulipofika mapokezi, uandikishaji ulifanyika haraka ambapo nilipelekwa kwenye chumba cha Ajali na Dharura. Madaktari walinichunguza na kubaki na mimi kwa usiku mzima, ikiwa ni pamoja na mwanangu Bis (Bisala).

Asubuhi, kunako saa moja madaktari waliamua kwamba walikuwa wamefanya kila waliloweza, hivyo walinipeleka katika kitengo cha uangalizi wa karibu zaidi (High Dependence Unit – HDU) ambacho si cha wagonjwa mahututi. Huko nilipokelewa na timu nyingine ya madaktari ambao kila mtu alifanya uchunguzi wake kufahamu tatizo nililokuwa nalo.
Kunako saa mbili asubuhi, madaktari walimwambia Bis aende nyumbani akapumzike. Kwa vile alikuwa amechoka kwa kukaa macho usiku mzima ikiwa ni pamoja na wasiwasi wa kunihudumia, alikubaliana nao.


Hata hivyo, mara tu aliposhikwa usingizi, simu yake ya mkononi ikalia. Ilikuwa kunako saa nne na nusu Jumamosi ya tarehe 6. Madaktari walimpigia simu arejee hospitalini kwa vile hali yangu ilikuwa imezidi kuwa mbaya.
Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wa kisa hiki cha kweli kwenye mtanadao huu huu wa tanzanialeo.com siku ya Jumatano.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment