Serikali
imesema kuanzia sasa mtumishi wa umma atakayeshindwa kusimamia
rasilimali za umma, achague moja kati ya mawili, kuacha kazi au
atumbuliwe.
Hayo
yalisemwa jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakati
alipozindua kitabu cha mwongozo wa usimamizi wa rasilimali za umma
unaolenga kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa na kusimamiwa
vizuri kwa maslahi ya Taifa.
Dk
Mpango alizindua kitabu hicho jana katika ukumbi wa Hazina mjini Dodoma
na baadaye semina elekezi iliyoandaliwa na Tume ya Mipango ilitolewa
kwa watumishi wa Serikali.
Akizindua kitabu hicho, Dk Mpango alisisitiza kuwa mtumishi atakayeshindwa kuendana na maelekezo hayo ‘atatumbuliwa’.
“Mkishindwa
kusimamia miradi kuna mawili, muache kazi mapema kama hamuwezi
usimamizi au tuwatumbue, katika hilo hatutasita,” alisema
Katika
ufafanuzi wake, Dk Mpango alisema katika bajeti ya Serikali mwaka
2016/17, fedha za maendeleo zilizotengwa ni asilimia 40 ya bajeti yote,
hivyo lazima iwekwe mikakati ya kuhakikisha miradi ya maendeleo
inasimamiwa kabla na baada ya kukamilika.
“Kwenye
masoko ya fedha na mitaji zipo fedha nyingi, lakini ili mwekezaji
awekeze kwenye mradi ni lazima mradi husika uwe umeandaliwa vyema,”
“Hapa
nchini kwetu tumekuwa na tatizo la muda mrefu la kuwa na miradi ambayo
haijaandaliwa vizuri kwa hiyo tunakosa fursa ya kufikia masoko ya
mitaji,” alisema Dk Mpango.
Alisema
kitabu hicho ni muongozo wa wataalamu na wadau wote ili kuiwezesha nchi
kuandaa miradi mizuri, kufuatilia utekelezaji wake ili iweze kuwasaidia
wananchi.
“Haiwezekani
tuendelee kulima mahindi na kuuza mazao hayo bila kuyaongezea thamani,
haiwezekani watu wachukue dhahabu na sisi kubaki na mashimo,” alisema.
Dk
Mpango aliwaonya watumishi umma waliokuwa katika uzinduzi huo kwamba
kuanzia sasa wana dhamana kubwa kwa Watanzania kuhakikisha dhamira ya
Serikali ya kuweka fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo inazaa
matunda.
Alisema Tanzania inaweza kuwa nchi ya kipato cha kati kabla ya 2025 kama miradi yote itasimamiwa vizuri.
“Ili
nchi yetu iweze kubadilika na rasilimali ziwasaidie wananchi wetu ambao
bado ni masikini, jambo muhimu ni kuhakikisha miradi ya maendeleo
inatekelezwa vizuri. Ili itekelezwe vizuri lazima iandaliwe vizuri na
isimamiwe vizuri hilo limekuwa tatizo letu la muda mrefu,”alisema.
Kwa
upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Florence Mwanri
alisema lengo la semina hiyo ambayo iliwashirikisha wataalamu kutoka
wizara mbalimbali, Idara na Halmashari ni kuwajengea uwezo wa kutambua
kipi wanapaswa kukifanya.
“Lazima
wataalamu hawa ambao ndiyo wanapanga na kuisimamia miradi hiyo wajue
kipi wanapaswa kukifanya, Serikali mwaka ujao wa fedha asilimia 40
zimepangwa kupelekwa katika miradi ya maendeleo sasa tukiwajengea uwezo
wataweza kuisimamia vyema na kupanga miradi yenye tija,”
“Wafadhili
wa miradi ya maendeleo wapo wengi, lakini tulikuwa tunashindwa
kuisimamia kwani hapakuwa na mipango na usimamizi mzuri, lakini Serikali
ya Rais Magufuli ambayo imeelekeza nguvu katika miradi ya maendeleo
bila shaka itawashughulikia watakaoshindwa kwenda na kasi.” alisema
Mwanri.
Mchumi
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Wilhem Ngasamiaku alisema baadhi ya
miradi inashindwa kutekelezwa kwa ufanisi kutokana na wasimamizi
kutokuwa na uelewa wa kutosha.
Alisema
kufanyika kwa semina hiyo sambamba na maelekezo yaliyopo katika kitabu
hicho, yatasaidia kuwawezesha wataalamu wa usimamizi wa miradi hiyo kuwa
na uelewa na jinsi ya kutoa kipaumbele, kuisimamia ili iwe na ufanisi.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment