Katibu
Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad ameendelea kumtupia lawama Rais mstaafu
wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete akidai kuwa alitumia dola ‘kupindua’
demokrasia ili kuinusuru CCM iliyokuwa imebwagwa kwenye Uchaguzi Mkuu
uliopita.
Alisema
Kikwete ambaye wakati huo alikuwa Amiri Jeshi Mkuu, anastahili lawama
kwa madai kuwa alituma vyombo vya dola kugeuza uamuzi wa Wazanzibari
waliokuwa wameufanya kupitia masanduku ya kura Oktoba 25 mwaka jana.
Maalim
Seif aliyasema hayo jana pale wananchi walipomtaka kutoa neno la
kuwasalimu alipopita katika Msikiti wa Ijumaa wa Masjid Swahaba, Mtoni
Garagara, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
“Kilichofanyika
si kitendo cha kiungwana hata kidogo, ni uhuni wa hali ya juu
uliopangwa kwa makusudi na watu wasioitakia mema Zanzibar na hivyo
wakaamua kutoheshimu haki na uamuzi halali wa wananchi,” alisema.
Maalim Seif alisema nchi ni mali ya wananchi ambao siku zote watabaki kuwa sehemu muhimu ya uamuzi wa nani awaongoze.
Katibu
mkuu huyo ambaye alikuwa mgombea wa urais wa Zanzibar katika uchaguzi
huo, alisema watawala wanapaswa kutambua wananchi ndiyo huamua watu
wanaowataka na siyo mabavu ya kulazimisha kwa kutumia dola au majeshi.
Hata
hivyo, Maalim Seif alisema anaelewa hali ilivyo katika jamii na pia
katika mioyo za Wazanzibari ambao uamuzi wao ulipinduliwa.
Maalim
Seif aliyedai kushinda nafasi hiyo, aliwataka Wazanzibari kuendelea
kuwa watulivu wakielewa kuwa wao ndiyo washindi na ushindi hautapotea.
Mwanasiasa huyo alisema juhudi zinaendelea kuhakikisha haki ya uamuzi wao kupitia masanduku ya kura inapatikana.
Wananchi
walioibuka kwa wingi katika eneo hilo baada ya kubaini sauti iliyokuwa
ikizungumza kwenye kipaza sauti ni ya Maalim Seif, walielezea
kufurahishwa na kiongozi huyo.
“Tumejisikia furaha angalau kusikia sauti ya simba wa nyika, Maalim Seif akinguruma,” alisema mkazi wa Mtoni Kidatu, Bura Juma.
Slim Said alisema: “Unajua Maalim ni kipenzi cha watu, sasa ukimsikia tu unaondoka na hisia za matumaini.”
Msafara
huo wa Maalim usiokuwa na king’ora kama ilivyozoeleka ulionekana
ukiingia taratibu, hali ambayo haikuamsha shangwe mwanzoni kabla ya watu
kupashana habari na hatimaye kujaa mahali alipokuwa.
Uchaguzi
Mkuu wa mwaka jana ulitawaliwa na mvutano wa kisiasa visiwani Zanzibar
baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim
Jecha kufuta matokeo akidai kuwa sheria na taratibu zilivunjwa. Kutokana
na hatua hiyo, baadaye Jecha alitangaza uchaguzi wa marudio Machi 20
mwaka huu ambao uligomewa na vyama 10 kati ya 14 vilivyoshiriki uchaguzi
wa awali.
Katika uchaguzi wa marudio, Dk Ali Mohamed Shein alishinda kwa asilimia 91.4.
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
[MATUSI HAYARUSIWI]
0 comments:
Post a Comment