YANGA SC Yanasa Siri 5 za Waarabu wa Al Ahly ya Misri

pluijm1Kocha mkuu wa Yanga Hans van Pluijm.
Nicodemus Jonas na Omary Mdose
NI rasmi sasa Yanga itakutana na Waarabu wa Misri, Al Ahly katika raundi ya pili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya timu zote kufuzu juzi Jumamosi.
Yanga walifuzu mbele ya APR huku Al Ahly wao wakitinga hatua hiyo kwa kuichapa FC Libolo ya Angola mabao 2-0. Mchezo wa kwanza zilitoka suluhu.

Hii itakuwa mara ya tatu ndani ya miaka 10 Yanga kukutana na Waarabu hao huku ikiwa na takwimu ya kuondolewa kila wanapokutana nao.

Hata hivyo, huenda hii ikawa safari ya kwanza kwa Yanga kuwaondoa kutokana na kasi ya Yanga ilivyo ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Kwa taarifa yako tu, Yanga ndiyo wanapeperusha bendera ya Ukanda wa Afrika Mashariki kwenye hatua hii katika nchi tano zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mechi ya kwanza itapigwa Aprili 9 na marudio ni wiki zijazo.

Hata hivyo, ili kufuta rekodi mbaya mbele ya Al Ahly, kocha Hans van Pluijm lazima atilie maanani siri tano zifuatazo.

Umakini kipindi cha pili
Takwimu zinaonyesha katika mechi 10 za Al Ahly za hivi karibuni, mechi nane wamepata mabao yao kipindi cha pili huku mbili zilizosalia wakitoa suluhu. Hii lazima iwe tahadhari kwa Yanga ambayo katika mechi mbili za mwisho dhidi ya APR ya Rwanda kwenye michuano hii, ilionekana kupungua kasi kwa kiasi kikubwa kipindi cha pili.

Fowadi kali, beki ukuta wa Berlin
Al Ahly ndiyo vinara wa Ligi ya Misri wakiwa na pointi 47, sita mbele ya Zamalek inayoshika nafasi ya pili, lakini pia ndiyo timu yenye fowadi kali na beki bora. Wamefunga mabao 35 katika mechi 21 walizocheza mpaka sasa na kuruhusu mabao 14 ambayo ni machache zaidi.

Takwimu mbaya kuihukumu Yanga?
Katika awamu nne za hivi karibuni, Yanga ilizokutana na timu kutoka Uarabuni, haijawahi kuitoa timu yoyote, lakini angalau mwaka 2014 ilionyesha mwanga baada ya kushinda 1-0 Taifa na kutolewa kwa penalti katika mechi ya pili.
Katika hilo, Pluijm amesema: “Tunahitaji kufanya maandalizi kwelikweli, mechi itakuwa ngumu.”

Wastani wa mabao
Kidogo inaweza kuwa nafuu kwa Yanga kwani inaonekana Yanga ina wastani wa kufunga mabao mengi
kuliko Al Ahly ambayo wastani wake ni mabao mawili, lakini ngumu kuruhusu bao. Katika mechi 10 za mwisho, imeruhusu mabao manne tu na kufunga mabao 12.

Kocha wao ni noma
Al Ahly wanakuja nchini wakiwa na kocha mzoefu aliyefundisha timu kadhaa za Ligi Kuu England kama Tottenham, Fulham na Ajax ya Uholanzi na Hamburger SV ya Ujerumani. Anaitwa Martin Jol. Kocha Pluijm amesema: “Namjua tangu akiwa Uholanzi. Ni kocha bora na ana mbinu bora kutokana na kwamba amefundisha timu kubwa lakini siku zote unapocheza dhidi ya timu kubwa hautakiwi kuogopa bali kuziheshimu.”

Kocha APR adai Yanga itawafunga Waarabu…
Kocha Mkuu wa APR ya Rwanda, Nizar Khanfir, raia wa Tunisia, amewatoa hofu wapenzi na mashabiki wa Yanga kwa kusema kwa jinsi Yanga inavyocheza, ana imani itaifunga Al Ahly.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Khanfir alisema Yanga imekuwa ikibadilika kulingana na timu inayokutana nayo, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kufika mbali zaidi ya ilipo sasa ikichagizwa na kuwa na wachezaji wengi wazoefu.

“Tayari tumetolewa na naipongeza Yanga kwa kupita na kuingia hatua inayofuata, ni matumaini yangu kuwa Yanga itafika mbali zaidi kutokana na kucheza kwao kwa kujitambua, wana wachezaji wazoefu, pia wanabadilika kulingana na wakati, hivyo hatua waliyoingia wanaweza kuvuka,” alisema Khanfir
TUPE MAONI YAKO HAPO CHINI
[MATUSI HAYARUSIWI]
Share on Google Plus
    Facebook Comment
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment